
Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imewahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya kilimo cha bustani (Horticulture), hususan uwekezaji katika uzalishaji, uhifadhi, usafirishaji na uongezaji thamani wa mazao.
Meneja Uhamasishaji wa Uwekezaji wa nje kutoka TISEZA, Daudi Riganda, amesema sekta hiyo inayojumuisha maua, matunda, mbogamboga na viungo inaendelea kuwa na fursa za kiuchumi kupitia mauzo ya nje na kuvutia mitaji, huku akitaja uwekezaji katika umwagiliaji, maghala, vyumba vya ubaridi (Cold Rooms), vituo vya kuhifadhi mazao (Cold Stores) na viwanda vya kuongeza thamani.
Akizungumza katika Maonesho ya Hortilogistical Africa 2026, Riganda amesema TISEZA imeshiriki kutoa elimu na kuhamasisha uwekezaji, huku ikitumia kituo cha huduma za pamoja (One Stop Center) kinachojumuisha taasisi takribani 15 za Serikali kuwezesha wawekezaji kupata huduma sehemu moja badala ya kufuata taasisi mbalimbali, amesema mwekezaji anayekidhi vigezo na kukamilisha nyaraka zinazohitajika anaweza kupata cheti cha uwekezaji ndani ya saa 24.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa masharti aliyoyataja, Mtanzania anahitaji mtaji wa takribani Sh milioni 150, sawa na Dola za Marekani 50,000, huku mwekezaji wa kigeni au ubia akihitaji Dola za Marekani 500,000, akiwahimiza Watanzania kutumia fursa zilizopo katika sekta hiyo.
Kwa upande wa Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo, mwakilishi wake amesema moja ya malengo yanayohamasishwa kupitia maonesho hayo ni kupunguza upotevu wa mazao ya bustani baada ya mavuno kutoka asilimia 40 hadi asilimia 20, kupitia uwekezaji katika miundombinu ya uhifadhi na uongezaji thamani. Fursa hizo zinahusisha mazao ya kimkakati yakiwemo parachichi, ndizi, zabibu na viungo.
Naye Nasrul Salum Nasrul kutoka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), amesema ushiriki wao katika kituo hicho unalenga kuwaunganisha wazalishaji na masoko ya ndani, kikanda na kimataifa, pamoja na kukuza wajasiriamali wadogo ili waweze kupanua biashara zao na kufikia masoko makubwa.
Kwa upande wake, Tulibako Minga kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), amesema kituo hicho kinatoa huduma kwa wadau wa mnyororo wa thamani wa Horticulture, kuanzia uzalishaji, biashara ya ndani na nje ya nchi hadi usafirishaji wa mazao.
Naye Mdili Katemani kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), amesema mamlaka hiyo inasaidia kufungua masoko mapya ya kimataifa, kukagua mazao yanayosafirishwa nje ya nchi na kutoa cheti cha afya ya mimea (Phytosanitary Certificate), huku ikiwawezesha wakulima kupata taarifa na kutimiza masharti ya masoko ya kimataifa.



TAFUTA HABARI
Social Plugin