Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIJANA WAHAMASISHWA KUSHIRIKI KATIKA UZALISHAJI WA MAZAO YA MBOGAMBOGA, MATUNDA, MAUA NA VIUNGO


 Vijana wamehamasishwa kushiriki kikamilifu katika uzalishaji katika sekta ya kilimo, hususani kwenye mazao ya bustani ambayo yana fursa nyingi katika mnyororo wa thamani.

Hayo yamesemwa na washiriki wa Maonesho ya Kimataifa ya HortiLogistica yanayoendelea Jijini Arusha.

Mshiriki wa maonesho hayo, Ndugu Baraka Jeremia Chijenga, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilimo Fresh ambayo Makao Makuu yake yapo Jijini Dar es Salaam, eneo la Mwenge, amesema kampuni hiyo inajihusisha na ununuzi wa mazao ya horticulture kutoka kwa wakulima hapa nchini na kuyauza hapa nchini.

Amewataka vijana kushiriki katika uzalishaji, akisema sekta ya kilimo ina fursa nyingi katika mnyororo wa thamani hususani kwenye mazao ya bustani.

Aidha, amewataka vijana wasiogope changamoto katika kilimo, kwani hata yeye alipoanza kilimo alikumbana na changamoto ya masoko, jambo ambalo aliligeuza kuwa fursa iliyosababisha kuanzisha Kampuni ya Kilimo Fresh.

Amesema kampuni hiyo kwa sasa inasaidia kutoa mafunzo kwa vijana ambao wako tayari kushiriki katika tasnia hiyo.

Akitoa mfano, amesema tayari ametoa mafunzo kwa vijana kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wanaotaka kujikita katika tasnia hiyo kwa kushirikiana na SUGECO. Amewahimiza vijana kuwa zipo fursa nyingi katika kilimo, wasiogope.

Naye Ndugu Dustin kutoka Kampuni ya Shambalai yenye ofisi zake mkoani Arusha, Mbuguni, Wilaya ya Arumeru, ambaye ni miongoni mwa vijana, amewataka vijana kuchangamkia fursa, akitoa mfano wa zao analolisafirisha na ambalo lina soko kubwa kuwa ni zao la tango poli, ambalo kwa sasa wanalisafirisha kwenda nchi za Ulaya.

Amesema zao hilo lina sifa ya kustawi katika maeneo yenye mvua chache, hivyo linaweza kulimwa katika maeneo mengi hapa nchini.

Amewakaribisha vijana kwenda kujifunza kuhusu uzalishaji wa zao hilo na upatikanaji wa soko lake.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com