Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Jiji la Dodoma linatarajiwa kupanuka kwa kasi kupitia mpango wa ujenzi wa mji mpya wa kisasa wa Hombolo, baada ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kusaini mkataba na kampuni ya kimataifa ya Heerim Architecture & Planning kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mradi huo.
Mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuendeleza Jiji la Dodoma ili liendane na hadhi ya Makao Makuu ya Nchi, kwa kuimarisha mipango miji, kuvutia uwekezaji na kupanua wigo wa huduma za kijamii na kiuchumi.
Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kuzindua majengo na miundombinu ya Mji wa Serikali Mtumba, ambapo alitoa maelekezo kwa viongozi kuhakikisha Dodoma inaendelea kuimarika kwa kuwa na hadhi na huduma zinazolingana na nafasi yake ya kitaifa.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba huo leo November 9,2026 Jijini hapa,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyemule, amewataka watendaji wa Halmashauri ya Jiji kuhakikisha wanajiandaa kikamilifu kusimamia mradi huo ili kazi zinazopangwa zitekelezwe kwa wakati na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
"Wakati Dodoma ikiendelea kuimarisha hadhi yake kama Makao Makuu ya Nchi, Hombolo inatarajiwa kuwa miongoni mwa maeneo yatakayobeba sura mpya ya ukuaji wa jiji hilo kupitia mpango wa kuanzisha mji wa kisasa wa Hombolo Thematic City,"ameeleza
Pia amesema utekelezaji wa mpango huo ni sehemu ya juhudi za kuendeleza Dodoma kwa kuimarisha mipango miji, kuvutia uwekezaji na kupanua huduma za kijamii na kiuchumi, ili kukidhi mahitaji yanayoendana na hadhi ya makao makuu.
Ili kufanikisha hilo ,Mkuu huyo wa Mkoa amewataka watendaji wa Halmashauri ya Jiji kuhakikisha wanajiandaa kikamilifu kusimamia mradi huo ili kazi zilizopangwa zikamilike kwa wakati na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Senyemule amesema maandalizi na usimamizi madhubuti ni muhimu katika kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia matarajio yaliyowekwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dk. Frederick Sagamiko, amesema mradi huo umepangwa kutekelezwa kwa ushiriki mkubwa wa sekta binafsi, ambayo inatarajiwa kuchangia asilimia 70 ya ujenzi wake.
Amesema dhana iliyotumika kuanzisha mradi huo inalenga kuweka mazingira yatakayowezesha sekta binafsi kushiriki katika uendelezaji wa mji huo, hatua inayotarajiwa kuongeza kasi ya uwekezaji na kupanua shughuli za kiuchumi.
Naye Msimamizi wa Mradi huo, William Azori, ameeleza kuhusu hatua za maandalizi na utekelezaji wa mpango huo, akibainisha umuhimu wa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika kuweka msingi wa ujenzi wa mji huo wa kisasa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Heerim Architecture & Planning, Young-in Jung, amesema kampuni hiyo imejipanga kutekeleza kazi hiyo kwa ufanisi, akieleza kuwa upembuzi yakinifu unaweza kukamilika kabla ya muda uliopangwa iwapo watapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wadau wanaohusika.
Wakati viongozi na wataalamu wakiweka msingi wa utekelezaji wa mradi huo, wananchi wa Kata ya Hombolo Bwawani wameeleza utayari wao wa kuupokea, wakitarajia kuwa uwepo wake utafungua fursa mbalimbali zitakazochochea maendeleo ya eneo hilo.
Hawa Bernard anasema wananchi wanatarajia mradi huo kuongeza fursa za ajira kwa vijana, kukuza biashara ndogondogo, kuvutia uwekezaji na kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii, ambazo kwa pamoja zinaweza kuchangia kuinua hali ya maisha ya wakazi wa eneo hilo.
Amesema uwekezaji utakaovutwa na mradi huo unaweza kuongeza shughuli za kiuchumi na kutoa nafasi kwa wananchi kushiriki katika fursa zitakazojitokeza, badala ya kubaki watazamaji wa mabadiliko yanayotarajiwa katika eneo lao.
Aidha, wameeleza umuhimu wa kushirikishwa katika hatua za utekelezaji wa mradi ili kuhakikisha matarajio ya wakazi yanazingatiwa na manufaa ya maendeleo yanawafikia wananchi wa Hombolo na maeneo jirani.
Mradi wa Hombolo Thematic City unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Novemba 9, 2026, hatua inayoweka matarajio mapya kuhusu mwelekeo wa ukuaji wa Dodoma na nafasi ya maeneo ya pembezoni katika maendeleo ya Makao Makuu ya Nchi.
Kwa kuzingatia hatua ya sasa ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, macho ya wananchi sasa yanaelekezwa katika matokeo ya maandalizi hayo na namna yatakavyogeuzwa kuwa utekelezaji wenye manufaa kwa jiji na wakazi wake.







TAFUTA HABARI
Social Plugin