Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YACHUKUA HATUA KUMALIZA MGOGORO WA SHAMBA LA TVLA MIVUMONI

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kigurusimba, Wilaya ya Pangani mkoani Tanga (hawapo pichani), Novemba 3, 2026, kuhusu hatua za kutatua mgogoro wa muda mrefu wa uvamizi wa Shamba la Serikali la Utafiti na Mifugo Mivumoni, linalosimamiwa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

***************

-TAKUKURU yaagizwa kuchunguza ugawaji wa ardhi, shughuli za ujenzi na kilimo zasitishwa

Na Daudi Nyingo – Tanga

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, ameagiza kuhakikiwa kwa mipaka na kusitishwa kwa shughuli za uendelezaji katika eneo la mgogoro wa muda mrefu wa uvamizi wa Shamba la Serikali la Utafiti na Mifugo Mivumoni, linalosimamiwa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ili kutatua mgogoro wa muda mrefu wa uvamizi unaohusisha wananchi wa Kijiji cha Kigurusimba, Wilaya ya Pangani.

Akizungumza na wananchi kijijini hapo Novemba 3, 2026 amesema ndege nyuki (drone) zitatumika kupata picha za hali ya eneo kabla ya wataalamu kuweka alama za mipaka na kubainisha majengo yaliyo ndani ya shamba na pia ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza namna maeneo hayo yalivyogawiwa, huku TVLA ikithibitisha kuachia hekta 1,271 kati ya hekta 5,320 kwa Serikali ya Kijiji kwa ajili ya kuwagawia wananchi.

“Namaliza kikao hiki naachia kazi TAKUKURU. Wapitie wote waliopata haya maeneo na wajue kitu gani kilitokea na kama kulikuwa na rushwa katika upatikanaji wa eneo. Waliosababisha hali hiyo ni lazima tuwachukulie hatua.”

“Katazo la uendelezaji wa aina yoyote, iwe ni kilimo, iwe ni ujenzi, nawaomba sana yote yasimamishwe. Lakini mtu asiende akaamua kuhamia kwenye eneo lililobaki kabla hajapangwa, kwa sababu unaweza ukaja kuondolewa. Haya mambo yanapangwa kupitia ramani,” amesema Mhe. Balozi. Dkt. Batilda.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TVLA, Dkt. Stella Bitanyi, amesema Wakala ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Mkoa kumaliza mgogoro huo na wataalamu wa TVLA watashiriki katika uhakiki wa waliopo ndani na nje ya mipaka ya shamba, pamoja na kutambua maeneo yatakayobaki kwa shughuli za taasisi, ikiwemo ufugaji na kilimo cha malisho.

“Ni mgogoro wa muda mrefu, na imekuwa ni mawasiliano ya muda mrefu kutatua hili. Tuko tayari kushirikiana katika kuona kwamba mgogoro huu unaisha na wananchi wanaishi salama. Tunaafiki kuundwa kwa kamati na tuko tayari kuanza kazi wiki inayoanza tarehe 9 Novemba, kupitia na kuona ni nani aliyeko ndani, ni nani aliyeko nje na wapi tunaweka alama za mipaka,” amesema Dkt. Bitanyi.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Bw. Rashid Kassim Mchatta, amesema timu ya wataalamu itakayoundwa itajumuisha wataalamu kutoka Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na TVLA, ili kutekeleza maelekezo ya kuhakiki mipaka na masuala ya upimaji na hati.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigurusimba, Bw. Silvesta Mango, amekiri kuwa baadhi ya wananchi wako ndani ya eneo la shamba, akieleza kuwa walipewa maeneo hayo na Serikali ya Kijiji. Ameomba kuangaliwa uwezekano wa kubakiza sehemu ndogo ya eneo lenye makazi katika Kitalu Namba Nne, ambako wananchi wamejenga nyumba na kuweka miundombinu, ikiwemo umeme.

Kwa upande wa wananchi, Mama Mnyetama ameiomba Serikali kusaidia kupima na kuweka alama za mipaka katika maeneo yao yaliyo nje ya Shamba la Utafiti na Mifugo Mivumoni, ili wawe na uhakika wa umiliki na kuepuka migogoro mingine ya ardhi. Amesema hatua hiyo itawasaidia kutambulika kuwa wamiliki halali na kuendesha shughuli zao kwa utulivu.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi, akizungumza katika kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, na wananchi wa Kijiji cha Kigurusimba, Wilaya ya Pangani mkoani Tanga, Novemba 3, 2026, kuhusu utayari wa Wakala kushirikiana na Serikali ya Mkoa kutatua mgogoro wa muda mrefu wa uvamizi wa Shamba la Serikali la Utafiti na Mifugo Mivumoni.
Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Mhe. Mwanaidi Rajabu, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kigurusimba na kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, katika kikao kilichofanyika kijijini hapo, Novemba 3, 2026, kujadili hatua za kutatua mgogoro wa muda mrefu wa uvamizi wa Shamba la Serikali la Utafiti na Mifugo Mivumoni, linalosimamiwa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA).
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Bw. Rashid Kassim Mchatta, akizungumza katika kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, na wananchi wa Kijiji cha Kigurusimba, Wilaya ya Pangani mkoani Tanga, Novemba 3, 2026, kuhusu kuundwa kwa timu ya wataalamu itakayohakiki mipaka na kushughulikia masuala ya upimaji na hati ili kutatua mgogoro wa muda mrefu wa uvamizi wa Shamba la Serikali la Utafiti na Mifugo Mivumoni.

Matukio mbalimbali katika picha yakionesha wakazi wa Kijiji cha Kigurusimba, Wilaya ya Pangani mkoani Tanga, wakifuatilia maelezo ya viongozi wakati wa kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, na wananchi wa kijiji hicho, Novemba 3, 2026, kuhusu hatua za kutatua mgogoro wa muda mrefu wa uvamizi wa Shamba la Serikali la Utafiti na Mifugo Mivumoni, linalosimamiwa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com