
Ubora wa elimu katika shule za serikali unaendelea kung’ara! Shule ya Msingi Masunula iliyopo katika Jimbo la Itwangi, Wilaya ya Shinyanga, imeweka historia baada ya kuongoza orodha ya shule kumi bora za Wilaya ya Shinyanga (Serikali na Binafsi) katika Matokeo ya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) mwaka 2026, ikiwa ni ushahidi kuwa shule za Serikali zina uwezo mkubwa wa kutoa elimu bora na kuzalisha wanafunzi wenye matokeo ya kiwango cha juu.
Kwa mujibu wa orodha ya shule kumi bora iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Masunula imeibuka kinara kwa kupata wastani wa alama 285.5172, huku wanafunzi wake wote 29 waliofanya mtihani huo, wakiwemo wasichana 17 na wavulana 12, wakipata Daraja A (Bora), sawa na asilimia 100 ya ufaulu.
Mafanikio hayo yanaifanya Masunula kuwa mfano wa kuigwa katika utoaji wa elimu bora katika shule za Serikali, ikionesha kuwa kwa usimamizi mzuri, walimu wenye kujituma, nidhamu ya wanafunzi na ushirikiano wa wazazi, mafanikio makubwa yanawezekana.
MASUNULA YANG’ARA MASOMO YOTE SITA
Uchambuzi wa matokeo unaonesha kuwa wanafunzi wa Masunula wamefanya vizuri katika masomo yote sita, ambapo Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi limeongoza kwa wastani wa alama 49.5517 kati ya 50, likifuatiwa na Hisabati (49.5172), Uraia na Maadili (47.9310), Sayansi na Teknolojia (47.5862), English Language (46.8966) pamoja na Kiswahili (44.0345).
Jambo la kipekee ni kwamba masomo yote sita yameingia katika kundi la Daraja A (Bora), huku hakuna mwanafunzi aliyepata daraja la chini ya A katika matokeo ya jumla.
Hii ni taswira inayodhihirisha juhudi za walimu na wanafunzi katika kuhakikisha hakuna somo linaloachwa nyuma katika safari ya kutafuta mafanikio ya kitaaluma.
SHULE NYINGINE TISA ZA SHINYANGA ZILIZOINGIA 10 BORA
Mbali na Masunula, shule nyingine zilizofanikiwa kuingia katika orodha ya shule kumi bora za Wilaya ya Shinyanga kwa matokeo ya PSLE 2026 ni St. Maria Goretti iliyoshika nafasi ya pili kwa wastani wa alama 269.3846, Shilabela nafasi ya tatu (268.1852), Kimandaguli nafasi ya nne (266.3864), Salawe nafasi ya tano (262.3939), Ikonda nafasi ya sita (259.8571), Kilimawe nafasi ya saba (257.1875), Kihongwe nafasi ya nane (254.0714), OLA nafasi ya tisa (252.6667) na Sumbigu iliyoshika nafasi ya kumi kwa wastani wa alama 252.0000.
Matokeo hayo yanaonesha ushindani na juhudi za shule mbalimbali katika Wilaya ya Shinyanga katika kuboresha kiwango cha elimu na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
AZZA ATOA PONGEZI, AAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA SHULE
Akizungumza baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, amewapongeza walimu, wanafunzi, wazazi na viongozi wa shule kwa mafanikio hayo, akisema ni matokeo ya kujituma na ushirikiano katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad
Mhe. Azza amesema mafanikio ya Masunula yanapaswa kuwa chachu kwa shule nyingine katika Jimbo la Itwangi na Wilaya ya Shinyanga kwa ujumla kuendelea kuongeza juhudi katika kuboresha ufaulu.
“Ninaipongeza shule hii, kwa miaka mingi imeendelea kufanya vizuri katika mitihani ya taifa. Haya ni matokeo ya juhudi kubwa za walimu, wanafunzi na wazazi. Kama Mbunge wenu, nitaendelea kushirikiana nanyi kuhakikisha miundombinu ya shule zetu inaboreshwa zaidi ili kila mwanafunzi wa Itwangi apate mazingira bora ya kujifunzia,” amesema Mhe. Azza.
Ameongeza kuwa matokeo hayo yanadhihirisha uwezo mkubwa wa Jimbo la Itwangi kufanya vizuri katika sekta ya elimu, endapo wadau wote wataendelea kushikamana katika kutekeleza mikakati ya kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
SHULE ZA SERIKALI NI CHAGUO LA ELIMU BORA
Mafanikio ya Masunula yanatoa ujumbe muhimu kwa wazazi na walezi kuwa shule za Serikali zina nafasi kubwa katika kujenga msingi imara wa elimu kwa watoto wao.
Ni wakati wa kuendelea kutambua, kuunga mkono na kuimarisha shule za Serikali kupitia ushirikiano wa Serikali, Halmashauri, viongozi wa maeneo husika, walimu, wazazi na jamii.
Kwa matokeo haya, Masunula imeonesha kuwa mafanikio makubwa ya kitaaluma yanawezekana na kwamba shule za Serikali zina uwezo wa kuandaa wanafunzi wanaoweza kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.
Hongereni Masunula! Hongereni walimu, wanafunzi, wazazi na wadau wote wa elimu katika Wilaya ya Shinyanga. Elimu bora ni msingi wa maendeleo ya jamii.



TAFUTA HABARI
Social Plugin