Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KABUDI AHIMIZA JAMII KUPINGA UNYANYAPAA KWA WANAOISHI NA VVU


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU), ikiwemo kupunguza maambukizi mapya kutoka watu 98,754 mwaka 2010 hadi 33,511 mwaka 2025.

Amesema katika kipindi hicho, vifo vinavyotokana na UKIMWI vimepungua kutoka watu 55,833 hadi 25,995, huku maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yakishuka kutoka asilimia 9.1 hadi 6.2.

Prof. Kabudi ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, yanayofanyika Desemba Mosi kila mwaka, ambapo mwaka huu yataambatana na kumbukumbu ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).

Amesema takwimu za mfumo wa taarifa za afya (DHIS-2) hadi Desemba 2025 zinaonesha kuwa asilimia 92.7 ya watu wanaoishi na VVU wanajua hali zao, asilimia 99.5 ya wanaofahamu hali zao wanapata dawa za kufubaza VVU (ARV), huku asilimia 98.2 ya wanaotumia dawa hizo wamefanikiwa kufubaza virusi mwilini.

Mafanikio hayo ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya 95-95-95 yanayolenga kuhakikisha asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wanajua hali zao, asilimia 95 ya wanaojua hali zao wanapata matibabu na asilimia 95 ya wanaotumia dawa wanafubaza virusi mwilini.

Aidha, Prof. Kabudi amesema utafiti wa Tanzania HIV Impact Survey (THIS) wa mwaka 2022/23 unaonesha kuwa Tanzania Bara ina kiwango cha maambukizi ya VVU cha asilimia 4.4, sawa na watu 1,690,948 wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wanaoishi na VVU.

Amesema Serikali itaendelea kuimarisha uwekezaji wa rasilimali za ndani, kuhamasisha sekta binafsi kushiriki katika mapambano hayo na kuendeleza ushirikiano na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha huduma za kinga, upimaji na matibabu zinapatikana kwa wananchi wote.

Alisisitiza umuhimu wa Tanzania kujenga uwezo wa kugharamia vipaumbele vyake vya kitaifa ili mabadiliko ya mazingira ya ufadhili wa kimataifa yasiathiri upatikanaji na mwendelezo wa huduma muhimu za VVU na UKIMWI.

Kuhusu maadhimisho ya mwaka huu, Prof. Kabudi amesema yataanza Novemba 24 hadi Desemba Mosi, 2026 katika kanda zote saba za TACAIDS ambazo ni Mashariki, Kati, Ziwa, Kusini, Nyanda za Juu Kusini, Magharibi na Kaskazini.

Amesema katika kanda hizo kutakuwa na shughuli za uhamasishaji kuhusu afua za UKIMWI, utoaji wa elimu na huduma mbalimbali za afya kwa wananchi, huku maadhimisho ya kitaifa yakianza Novemba 29 katika viunga vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Convention Centre, Dodoma.

Amesema kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika Desemba Mosi, 2026, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.

Maadhimisho hayo yatafanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Huduma Bora za Afya ni Msingi wa Kutokomeza UKIMWI, Tuendelee Kuimarisha Upatikanaji,” inayohimiza upatikanaji wa huduma, rasilimali na utashi wa kisiasa katika kuimarisha mwitikio wa Taifa dhidi ya VVU na UKIMWI.

Kwa mujibu wa Prof. Kabudi, maadhimisho hayo pia yanalenga kuwakumbuka waliopoteza maisha kutokana na UKIMWI, kuwaenzi wanaoishi na VVU, kutathmini hali na mwelekeo wa mapambano dhidi ya ugonjwa huo na kuhamasisha jamii kuendelea kushiriki katika ajenda ya kutokomeza UKIMWI.

Amesema maadhimisho hayo yatatoa fursa kwa Watanzania kutathmini mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 25 ya TACAIDS, changamoto zilizopo na mikakati ya kuimarisha mapambano dhidi ya UKIMWI kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Katika hotuba yake, Prof. Kabudi ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha sekta ya afya kupitia ujenzi wa vituo vya kutolea huduma, hospitali, ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, pamoja na kuboresha upatikanaji wa dawa za ARV zinazotolewa bila malipo.

Aidha, ametoa wito kwa Watanzania kutowanyanyapaa wala kuwabagua watu wanaoishi na VVU, badala yake kujenga jamii yenye upendo, mshikamano na inayowapa watu wote nafasi ya kuishi kwa utu na kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Amewataka pia vijana kuwajibika katika kujikinga na VVU, kupima ili kujua hali zao na kushiriki kutoa elimu sahihi kwa jamii.

Amesema takwimu zinaonesha kuwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wanachangia asilimia 33.3 ya maambukizi mapya ya VVU, huku asilimia 77.7 ya maambukizi mapya katika kundi hilo yakiwahusu vijana wa kike.

Prof. Kabudi amesisitiza kuwa jukumu la mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI ni la kila Mtanzania, akizitaka Serikali za mitaa, kamati za UKIMWI, asasi za kiraia, taasisi za dini, sekta binafsi na vyombo vya habari kuendelea kushirikiana katika kutoa elimu na kuimarisha mwitikio wa Taifa ili kufikia lengo la kutokomeza UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com