Makamu wa Rais wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ameitaka Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), kuweka mazingira yatakayowawezesha vijana wabunifu katika sekta ya kilimo kupata fursa za masoko, kufahamu viwango vya bidhaa na kuunganisha miradi yao na fursa za ufadhili ili kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Ametoa wito huo leo Novemba 9, 2026, wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Kilimo cha Mbogamboga, Maua na Matunda, yaliyowaleta pamoja washiriki kutoka Bara la Afrika, Ulaya na Asia (Hortilogistical Africa 2026), jijini Arusha, ambapo akisisitiza umuhimu wa Serikali na sekta binafsi kushirikiana kukuza ubunifu na biashara za vijana katika sekta ya kilimo.
Amesema vijana wanaojihusisha na uzalishaji wa mazao Mbogamboga na matunda, wanahitaji kuungwa mkono kwa kutambuliwa ubunifu wao, kuunganishwa na taasisi husika na kupata mwongozo wa viwango vya kimataifa vinavyohitajika kwa bidhaa mbalimbali zikiwemo kakao na parachichi ili ziweze kushindana katika masoko ya nje.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali inapaswa kukamilisha juhudi zinazofanywa na sekta binafsi kwa kuwaunganisha vijana na wadau wanaoweza kuwasaidia kuandaa maandiko ya miradi, kupata ufadhili na kufikia hatua ya utekelezaji wa miradi yao.
Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha ruzuku za pembejeo zinawafikia wakulima wenye uwezo wa kuzalisha kwa kuzingatia mahitaji ya soko, akitolea mfano wa miche 130,000 ya parachichi inayotolewa na Serikali na kuhoji iwapo inawafikia walengwa wenye uhakika wa soko la mazao hayo.
Kwa upande wake, Jofrey Ombeni Munisi kutoka kampuni ya Onocado Farm, ameishukuru Serikali kupitia COPRA na Shirika la TAHA kwa kuwawezesha wazalishaji kupata fursa za kutembelea maeneo mbalimbali na kushiriki shughuli za kibiashara ndani na nje ya nchi, akisema ushirikiano huo umemsaidia kukuza biashara yake katika masoko ya kimataifa na kufahamu viwango vinavyotakiwa.
Naye Hamza Mohammed Nangameta kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), amesema Tanzania inazalisha zaidi ya tani milioni 4 za ndizi kwa mwaka, zikiwemo aina za Malindi, Kisukari na Mzuzu, huku mikoa inayozalisha zao hilo ikiwa ni Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Njombe, Morogoro na Tanga. Ameongeza kuwa nchi inazalisha zaidi ya tani laki 8 za mananasi, yanayozalishwa katika mikoa ya Pwani, Mwanza, Geita, Morogoro na Mbeya.
Amesema Tanzania inaendelea kutumia fursa za masoko ya nje kwa kusafirisha ndizi katika nchi za Afrika Kusini, Uganda, Kenya, Malawi na Zambia, huku mananasi yakiuzwa Uganda na Visiwa vya Komoro, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha uzalishaji na biashara ya mazao hayo ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakulima na wafanyabiashara.




TAFUTA HABARI
Social Plugin