Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RUJAT YAPATA SAFU MPYA YA UONGOZI, NEVILLE MEENA ACHAGULIWA TENA KUWA MWENYEKITI


Baadhi ya viongozi wapya waliochaguliwa kuongoza Chama cha Waandishi wa Habari za Vijijini Tanzania (RUJAT) kwa kipindi cha miaka minne, katika Mkutano Mkuu uliofanyika jijini Dodoma. Picha na Debora Munisi
Mwenyekiti wa RUJAT, Neville Charles Meena, akizungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho jijini Dodoma baada ya kuchaguliwa tena kuongoza taasisi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka minne.
Mwenyekiti wa RUJAT, Neville Charles Meena, akizungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho jijini Dodoma baada ya kuchaguliwa tena kuongoza taasisi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka minne.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya RUJAT, Felix Mwakyembe, akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi wa viongozi wa chama hicho uliofanyika jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya RUJAT, Felix Mwakyembe, akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi wa viongozi wa chama hicho uliofanyika jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa RUJAT, Neville Charles Meena (kulia), akizungumza na Katibu wa chama hicho, Prosper Laurent Kwigize, wakati wa mkutano mkuu wa chama uliofanyika jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu Malunde 1 blog , Dodoma

MWANAHABARI mkongwe Neville Charles Meena amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Vijijini Tanzania (RUJAT), katika uchaguzi mkuu wa chama hicho uliofanyika jijini Dodoma, Oktoba 31, 2026.

Meena alitangazwa mshindi na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Felix Mwakyembe, katika uchaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Felix Mwakyembe

Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Meena alisema dhamana aliyopewa na wanachama ni wajibu mkubwa ambao anapaswa kuulipa kwa kuwatumikia kwa moyo wake wote.

Alisema ataendelea kusimamia malengo ya RUJAT, ikiwemo kuhakikisha habari zinazohusu wananchi wa vijijini zinapewa kipaumbele katika vyombo vya habari ili changamoto, fursa na shughuli mbalimbali za maendeleo zinazowahusu zipate nafasi inayostahili.

Meena alieleza kuwa atashirikiana na viongozi wenzake kuimarisha uwezo wa waandishi wa habari katika kuibua, kuandaa na kuandika habari zenye ubora na zinazogusa maslahi ya umma.

Meena amewahi kuwa Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na ana uzoefu mkubwa katika tasnia ya habari nchini.

Katika uchaguzi huo, Hamida Ramadhan kutoka Mkoa wa Dodoma amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa RUJAT, huku Prosper Laurent Kwigize kutoka Kasulu mkoani Kigoma akichaguliwa tena kuwa Katibu wa chama hicho.

Nafasi ya Mweka Hazina imechukuliwa na Zena Mohamed Chitwanga.

Aidha, wanachama wamewachagua wajumbe saba wa Kamati Tendaji ambao ni Musa Juma Siwayombe, Devotha Martine Paul, Kadama Malunde, Rashid Abdullah Mtagaluka, Anna Robi, Andrea Ashery Ngolole na Fadhili Abdallah Mwangamola.

Kwa mujibu wa mabadiliko ya Katiba yaliyopitishwa na wanachama wa RUJAT, viongozi waliochaguliwa watatumikia nafasi zao kwa kipindi cha miaka minne kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mwingine.

Uongozi huo mpya unatarajiwa kuendeleza juhudi za kukiimarisha chama, kuwaunganisha waandishi wa habari na kujenga uwezo wao kitaaluma, huku ukipa kipaumbele uandishi wa habari za vijijini unaolenga kuibua changamoto za wananchi, kuhamasisha uwajibikaji na kuchochea maendeleo ya jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com