
Na Kadama Malunde - Ushetu
Shule ya Msingi Nyabusalu iliyopo katika Jimbo la Ushetu, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, imeandika historia katika sekta ya elimu nchini baada ya kushika nafasi ya nne kati ya shule 10 bora Tanzania katika Matokeo ya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) mwaka 2026, huku wanafunzi wake wote 25 waliofanya mtihani huo wakipata Daraja A.
Mafanikio hayo yameongeza heshima kwa Jimbo la Ushetu na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla, huku Mbunge wa Jimbo hilo, Emmanuel Peter Cherehani, akipata sababu ya kujivunia maendeleo ya shule hiyo ambayo amekuwa karibu nayo katika kufuatilia na kuunga mkono juhudi za kuboresha elimu.
Kwa mujibu wa matokeo rasmi ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Shule ya Msingi Nyabusalu yenye namba PS1706083 imepata wastani wa alama 284.9200 na kushika nafasi ya nne kitaifa.
Katika matokeo hayo, wanafunzi wote 25 waliofanya mtihani wamepata Daraja A, wakiwemo wasichana 13 na wavulana 12, bila mwanafunzi aliyepata Daraja B, C, D au E.
Ukaribu wa Mbunge Emmanuel Cherehani na Shule ya Msingi Nyabusalu ni sehemu inayovutia katika safari ya maendeleo ya shule hiyo.
Januari 2026, Cherehani aliungana na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, kutembelea shule hiyo na kukabidhi mashine ya kuchapisha (printer) kwa ajili ya kusaidia shughuli za shule.
Katika ziara hiyo, Cherehani alieleza kuwa alikuwa amezungumza na mwalimu mkuu kuhusu changamoto zinazokabili shule hiyo, akitaja pia mipango ya kuboresha baadhi ya miundombinu ikiwemo nyumba za walimu na matundu ya vyoo katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Ushiriki huo unaonesha umuhimu wa viongozi kuwa karibu na taasisi za elimu, kusikiliza changamoto zake na kushirikiana na wadau wengine kutafuta suluhisho la mahitaji yanayokabili shule.
SHINYANGA YANG'ARA, SHULE TATU ZAINGIA TANO BORA KITAIFA
Mafanikio ya Nyabusalu yanaungana na matokeo mazuri ya shule nyingine mbili kutoka Mkoa wa Shinyanga zilizofanikiwa kuingia katika orodha ya shule tano bora nchini, hatua inayoufanya mkoa huo kuwa na shule tatu katika nafasi tano za juu.
Shule ya Msingi Masunula imeibuka nafasi ya pili kitaifa kwa wastani wa alama 285.5172, huku Shule ya Msingi Nyabusalu ikishika nafasi ya nne kwa wastani wa alama 284.9200 na Shule ya Msingi SAMUU ya Manispaa ya Shinyanga ikichukua nafasi ya tano kwa wastani wa alama 284.6800.
Masunula imefanya vizuri ikiwa na wanafunzi 29 waliofanya mtihani, SAMUU ikiwa na wanafunzi 75 na Nyabusalu ikiwa na wanafunzi 25. Wanafunzi wote katika shule hizo wamepata Daraja A, sawa na asilimia 100 ya ufaulu kwa kila shule.
Mafanikio hayo ni fahari kubwa kwa Mkoa wa Shinyanga, yakionesha uwezo wa shule zake kufanya vizuri katika ushindani wa kitaifa na kutoa hamasa kwa taasisi nyingine za elimu kuendelea kuimarisha viwango vya ufundishaji na ujifunzaji.
Kwa upande wa Ushetu, mafanikio ya Nyabusalu ni sababu ya pekee ya kujivunia, huku ukaribu wa Mbunge Cherehani na shule hiyo ukiendelea kuwa sehemu muhimu ya ushirikiano wa viongozi na taasisi za elimu.
Hongera Nyabusalu, hongera Masunula, hongera SAMUU, hongera walimu, wanafunzi, wazazi na wadau wote wa elimu wa Mkoa wa Shinyanga.


TAFUTA HABARI
Social Plugin