Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHILINGI BILIONI 379 KUIMARISHA UZALISHAJI WA MATALUMA YA RELI NCHINI



Na Sheila Ahmadi, Tabora

SERIKALI imeelekeza uwekezaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 379 katika kiwanda cha kutengeneza mataluma ya reli cha Uyumbu Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora katika juhudi za kuimarisha uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa kuagiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi ikiwemo China.

Hatua hiyo inalenga kuongeza uwezo wa Tanzania kuzalisha mataluma yanayohitajika katika ujenzi na matengenezo ya reli ya kisasa (SGR) na reli ya zamani (MGR) pamoja na kupunguza gharama zinazohusiana na upatikanaji wa bidhaa hizo.

Hayo yamesemwa Kaliua mkoani Tabora na Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ambapo amesema kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha sekta ya uchukuzi kwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa muhimu za reli nchini.

“kupitia Kiwanda hiki kitaongeza uzalishaji wa mataluma ya reli nchini na kupunguza utegemezi wa kuagiza kutoka nje huku Serikali imewekeza zaidi ya Sh bilioni 379 ikiwemo kodi ili kuhakikisha tunazalisha mataluma yatakayokidhi mahitaji ya reli zetu,” amesema Prof. Mbarawa.

Hatahivyo uzalishaji wa mataluma nchini unatarajiwa kusaidia kupunguza gharama za ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya reli, huku ukichangia kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa abiria na mizigo.

Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia kiwanda hicho ili kuhakikisha kinafikia malengo yaliyowekwa, hususan katika uzalishaji wa mataluma yenye ubora na kukidhi mahitaji ya sekta ya reli.

Aidha amesema uzalishaji huo una nafasi ya kufungua fursa mpya za kibiashara kwa Tanzania kupitia uwezekano wa kuuza mataluma katika nchi nyingine jambo linaloweza kuongeza mapato na mchango wa sekta ya viwanda katika pato la Taifa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Machibya Shiwa amesema kiwanda hicho kinatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha miundombinu ya reli na kuongeza ufanisi wa uendeshaji wa treni za MGR na SGR.

Amesema maboresho hayo yataimarisha huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo na kusaidia kuongeza mchango wa sekta ya reli katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

Kiwanda cha Uyumbu ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayolenga kuimarisha uzalishaji wa viwandani, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kujenga uwezo wa ndani wa kuhudumia mahitaji ya miundombinu ya uchukuzi nchini.















Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com