Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NIDA KIGEZO WAKULIMA KUPATA MBEGU ZA PAMBA- KISHAPU

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Josephati Limbe, akizungumza katika mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri wa kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika Kata mbalimbali kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 (Julai–Septemba). Oktoba 29, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Mkoa wa Shinyanga, Niceforus Mgaya, akizungumza kwenye mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika Kata mbalimbali kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 (Julai–Septemba) Oktoba 29, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu


Na Sumai Salum – Kishapu

Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga limeitaka Bodi ya Pamba kutafuta suluhisho la changamoto ya wakulima kukosa mbegu za pamba kutokana na kutokuwa na namba za utambulisho wa Taifa (NIDA), huku akitaka huduma za usajili wa NIDA zisogezwe karibu na wananchi wa vijijini.


Akizungumza kwenye barza hilo Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Josephat Limbe,Oktoba 29, 2026, kwenye mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya hiyo lenye lengo la kujadili utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo ya Kata kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 (Julai- Septemba), lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.


Amesema kutokuwa na namba za NIDA hakupaswi kuwa sababu ya mkulima kunyimwa mbegu za pamba, akionya kuwa hali hiyo inaweza kudhoofisha uzalishaji wa zao hilo muhimu kiuchumi., “Namba za NIDA isiwe kigezo cha wakulima kukosa mbegu za pamba. Bodi ya Pamba, tafuteni suluhisho mapema kuhakikisha wakulima wote wanapata mbegu kwa wakati, vinginevyo tunadhoofisha zao la pamba,” amesema Limbe.


Aidha Baraza hilo limeishauri NIDA kupeleka huduma za usajili katika Kata na Vijijini ili kuwawezesha wananchi kupata namba hizo kwa urahisi, akisisitiza kuwa NIDA ni nyaraka muhimu ya utambulisho wa Mtanzania katika huduma mbalimbali, si pembejeo za kilimo pekee.


Changamoto hiyo imeibuliwa kupitia taarifa za makatibu wa madiwani wa CCM na ACT-Wazalendo zilizowasilishwa barazani, zikibeba kero na maoni ya wananchi kuhusu upatikanaji wa pembejeo za kilimo na huduma za NIDA.


Katibu wa ACT-Wazalendo, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Bunambiyu, Mhe. Adrian Zengo, amesema wakulima wanahitaji huduma za usajili wa NIDA zisogezwe katika Kata zao kwa kuwa kufuatilia namba hizo katika Halmashauri ni gharama na kupelekea kuwa usumbufu unaoweza kuwanyima fursa ya kupata pembejeo.


Katibu wa Madiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Songwa, Mhe. Abdul Ngoromole, amesema wakulima wengi wanakosa mbegu kutokana na kutokuwa na namba za NIDA, akihofia kuwa hali hiyo inaweza kupunguza uzalishaji wa pamba na ali ya kulima zao hilo na matokeo yake Halmashauri na taifa kukosa mapato.


Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Seke Bogoro, Frednand Mpogomi, amesema baadhi ya wakulima hulazimika kutumia takribani Shilingi 20,000 kwa safari ya kufuatilia huduma za NIDA kwa umbali unaozidi kilomita 70 kutoka maeneo yao, hali inayowawia vigumu wananchi wa kipato cha chini.
Katibu wa Chama cha ACT Wazalendo na Diwani wa Kata ya Bunambiyu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Adrian Zengo (wa kwanza kushoto)
Katibu wa Madiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Songwa, Mhe. Abdul Ngoromole


Kwa upande wake Mkaguzi wa Bodi ya Pamba wilayani Kishapu, Joachim Gobanya, amesema ili mkulima akopeshwe mbegu za pamba anapaswa kuwa na namba ya NIDA nje na hapo atajaza fomu malumu itakayodhaminiwa na mkulima mwenzake mwenye namba ya NIDA na kisha kugongwa mhuri wa Mwenyekiti wa Kijiji na Afisa kilimo wa eneo husika kisha atasajiliwa kwenye mfumo wa Bodi ya pamba ili apewe mbegu nje na hapo mbegu hizo hazitatolewa.
Mkaguzi wa Bodi ya Pamba wilayani Kishapu mkoani shinyanga, Joachim Gobanya akitoa ufafanuzi kuhusu suala la NIDA na kupata mbegu za pamba kwa mkulima


Katika hoja nyingine, Diwani wa Kata ya Idukilo, Mhe. Sarah Marco, ameeleza kutoridhishwa na kutotekelezwa kwa mradi wa maji ya Ziwa Victoria unaotoka Mwaduhi Lohumbo na kupitia Nyenze, Mwang’olo na Kabila hadi Idukilo, akisema mradi huo ulianza mwaka 2023 lakini bado haujatekelezwa kama ilivyotarajiwa ili wananachi wapate huduma hiyo je ni lini RUWASA itakamilisha mradi huo?.


"Mhe. Mwenyekiti Kata ya Idukilo kiukweli ukosefu wa maji na huduma za kituo cha afya ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili wananchi, hivyo kupitia Baraza lako natamani nipate majibu ya uhakika ni lini mradi huo utakamilika maana taarifa ya RUWASA haioneshi mradi huo" Amesisitiza Sara
Diwani wa Kata ya Idukilo Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani shinyanga,Mhe. Sarah Marco akihoji kuhusu usogezaji huduma ya maji ya Ziwa Viktoria katika Kata hiyo kupitia mkutano wa Baraza la Madiwani


Akijibu swali hilo, Mhandisi wa Maji wa RUWASA Wilayani humo, John Lugembe, amesema utekelezaji wa miradi ya maji umekuwa ukikwamishwa na ufinyu wa bajeti, huku fedha zinazopatikana zikiwa hazitoshi kukamilisha miradi yote inayohitajika.


Wakichangia hoja hiyo, Madiwani wa Kata za Bubiki, Kishapu, Ukenyenge na Mwamashele wameishauri RUWASA kuweka kipaumbele katika kukamilisha miradi ya maji iliyoanzishwa kabla ya kuanzisha mingine mipya, wakieleza kuwa wananchi katika baadhi ya maeneo bado wanakabiliwa na ukosefu wa maji licha ya miradi kutajwa katika mipango ya utekelezaji.
Mhandisi wa Maji wa RUWASA Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, John Lugembe akijibu hoja za maji kwenye baraza hilo
Mwakilishi wa Ras Mkoa wa Shinyanga Ibrahimu Makana akizungumza kwenye mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri wa kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika Kata mbalimbali kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 (Julai–Septemba). Oktoba 29, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Enock Reuben, akifuatilia mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo wa kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika Kata mbalimbali kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 (Julai–Septemba) Oktoba 29, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com