Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Wakati macho na masikio ya Watanzania yakielekezwa jijini hapa kusubiri uzinduzi wa Mji wa Serikali Mtumba unaotarajiwa kufanywa kesho, Oktoba 30, 2026, waendesha bodaboda, bajaji na maguta wametembelea baadhi ya majengo ya serikali ili kufahamu huduma zinazotolewa na namna zitakavyowanufaisha wananchi.
Ziara hiyo imefanyika leo, Oktoba 29, 2026, imelenga kutambua majukumu ya baadhi ya wizara na namna wadau wa usafirishaji wanavyoweza kupata huduma katika mji huo ambao umejengwa kwa lengo la kuimarisha ufanisi wa shughuli za serikali.
Katika ziara hiyo, kundi hilo lilieleza dhamira ya kutembelea majengo matano yanayohusiana na shughuli zao za kila siku, likiwamo jengo la Wizara ya Maji, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara inayoshughulikia masuala ya vijana, Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Wizara ya Uchukuzi.
Akieleza sababu za ziara hiyo,Mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya boda boda,Guta na bajaji Tanzania Saidi Kagomba amesema wameamua kutembelea mji huo kabla ya uzinduzi wa ili kupata uelewa wa huduma zitakazopatikana na namna zitakavyoweza kuwafikia wananchi wa makundi mbalimbali.
Amesema wameona ni muhimu kufanya ziara hiyo kabla ya Rais kufanya uzinduzi , ili kupata maelezo ya kina kutoka kwa wataalamu kuhusu majengo na shughuli zitakazotekelezwa katika mji huo.
Akizungumza kwenye ofisi za Wizara ya Maji Mtumba,Kagomba amesema jengo la Wizara ya Maji ni muhimu kwa maisha ya kila siku ya wananchi, wakiwamo waendesha bodaboda, bajaji na maguta, ambao wanahitaji maji kwa ajili ya kunywa, kuoga na matumizi mengine ya nyumbani.
Kuhusu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, amesema wanatarajia kupata ufafanuzi kuhusu namna ofisi hiyo inavyoweza kusaidia kuboresha vituo vya bodaboda na bajaji, ikiwamo uwezekano wa kuwa na vituo vya kisasa vinavyokidhi mahitaji ya shughuli zao.
Ameongeza kuwa baada ya kutembelea Wizara ya Maji wanatarajia kwenda pia Wizara ya Uchukuzi ambayo ameitaja kuwa ni muhimu kwao kwa kuwa shughuli zao zinahusisha usafirishaji wa abiria na zinahitaji kufuata taratibu za kisheria, ikiwamo upatikanaji wa leseni zinazohitajika.
Aidha, walitaka kufahamu namna ya kupata msaada kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani na taasisi nyingine pale wanapokumbana na changamoto zinazohitaji uingiliaji wa serikali.
Akizungumza na kundi hilo, Fred Kaduma kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, amesema majengo ya Mji wa Serikali Mtumba yamekusudiwa kuhudumia watumishi wa serikali, viongozi pamoja na wananchi wa makundi mbalimbali.
Amesema ofisi hizo si kwa ajili ya viongozi na watumishi pekee, bali ni sehemu ya huduma za umma ambazo wananchi wanapaswa kuzifahamu na kuzitumia kulingana na mahitaji yao.
Kaduma amesema Ofisi ya Waziri Mkuu ina dhamana ya kuratibu uendelezaji wa Mji wa Serikali, huku akiwakaribisha wananchi kutembelea na kupata maelezo kuhusu shughuli zinazofanyika katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Paul Frank Nyongo, ambaye pia ni kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, amewapa waendesha bodaboda, bajaji na maguta maelezo ya awali kuhusu mji huo, akieleza kuwa eneo walilolitembelea ni sehemu ya mradi mkubwa wa Mji wa Serikali Mtumba.
Nyongo amesema ziara hiyo ni fursa kwa wananchi kufahamu historia ya mji huo, namna wazo lake lilivyoanza na hatua zilizofikiwa hadi kufikia maandalizi ya uzinduzi unaotarajiwa kufanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kesho.
Ameeleza kuwa kupitia maelezo ya wataalamu, wananchi wanaweza kuelewa zaidi namna mji huo ulivyopangwa na huduma zinazolenga kuboresha utendaji wa serikali.
Ziara hiyo imekuja katika kipindi ambacho maandalizi ya uzinduzi wa Mji wa Serikali Mtumba yanaelekea kukamilika, huku tukio la kesho likitarajiwa kuhusisha uzinduzi wa majengo ya serikali pamoja na barabara zilizojengwa ndani ya eneo hilo.
Ushiriki wa makundi kama waendesha bodaboda na bajaji katika ziara hiyo unaonesha umuhimu wa kutoa taarifa na elimu kwa umma kuhusu miradi ya kitaifa, ili wananchi wafahamu huduma zinazopatikana na namna wanavyoweza kuzifikia.
Mji wa Serikali Mtumba ni mradi muhimu kwa shughuli za Serikali jijini Dodoma, ambako uhamishaji na upangaji wa ofisi za serikali katika eneo moja unalenga kurahisisha uratibu wa shughuli za kiutawala na utoaji wa huduma kwa wananchi.




TAFUTA HABARI
Social Plugin