Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MTUMBA YAJIWEKA TAYARI KWA UZINDUZI WA KIHISTORIA



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

MAANDALIZI ya uzinduzi wa majengo ya ofisi za Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, yamefikia hatua ya kuridhisha kuelekea hafla ya kitaifa inayotarajiwa kufanyika kesho, Oktoba 30, 2026.

Hatua hiyo imebainika leo, Oktoba 29, baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, kufanya ziara ya kukagua maeneo yatakayotumika katika hafla hiyo.

Katika ziara hiyo, Prof. Mkumbo alikagua maeneo mbalimbali muhimu, yakiwemo geti kuu la kuingilia Mji wa Serikali, maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekaji mawe ya msingi ya majengo ya Serikali na barabara za lami, pamoja na Uwanja wa Mashujaa ambako hafla hiyo itafanyika.

Baada ya ukaguzi huo, Prof. Mkumbo alieleza kuridhishwa na hatua ya maandalizi iliyofikiwa, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo analolieleza kuwa la kihistoria kwa taifa.

Uzinduzi huo unatarajiwa kufanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa na mgeni maalum, Rais wa Jamhuri ya Angola, João Manuel Gonçalves Lourenço.

Hafla hiyo inatarajiwa kuashiria hatua muhimu katika matumizi ya majengo ya ofisi za Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na miundombinu ya barabara za lami iliyopo katika Mji wa Serikali Mtumba.

Katika ziara hiyo, Prof. Mkumbo aliambatana na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi; Naibu Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Dkt. James Kilabuko; Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali, Paul Sangawe, pamoja na maafisa wengine wa Serikali.









Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com