.jpeg)
Na Taikile Turo, Iringa
Mkoa wa Iringa umeeleza mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI baada ya kufikia asilimia 101-100-98 ya malengo ya kidunia ya 95-95-95 yanayolenga kudhibiti maambukizi ifikapo mwaka 2030, huku ukisisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za afya kupitia ushirikiano na wadau wa maendeleo.
Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Ufuatiliaji, Usimamizi na Ukaguzi, Helena Ntahema, aliyemwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa katika kikao cha uzinduzi wa mradi wa American First Global Health Strategy (AFGHS), unaotekelezwa na mashirika ya FHI 360 na JHPIEGO mkoani humo.
Ntahema amesema mkoa huo unatarajia ushirikiano na mashirika hayo utaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi, hususan katika maeneo ya VVU na UKIMWI, Kifua Kikuu, pamoja na afya ya mama na mtoto.
Ameipongeza FHI 360 kwa kuanza utekelezaji wa mradi huo katika afua za VVU na UKIMWI pamoja na Kifua Kikuu, huku akilishukuru shirika la JHPIEGO kwa kuhusika katika afua za afya ya mama na mtoto, akieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuimarisha huduma za afya na kufikia malengo yaliyowekwa.
Akieleza hali ya huduma za afya mkoani Iringa, Ntahema amesema mkoa una jumla ya vituo 359 vya kutolea huduma za afya, lakini ni vituo 285, sawa na asilimia 79, vinavyotoa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU (CTC), ambapo kati ya hivyo, vituo 147 pekee vilikuwa vinapata ufadhili kutoka kwa wadau.
Amesema takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma hizo ili ziweze kuwafikia wananchi kulingana na mahitaji yao, akisisitiza kuwa ushirikiano wa wadau unapaswa kuleta matokeo yanayopimika katika kuboresha huduma za afya.
Katika hatua nyingine, Ntahema amesema jumla ya vituo 285 vinatoa huduma za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT), akisisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma hizo ili wajawazito na wanawake wanaonyonyesha wapate huduma kwa wakati na watoto walindwe dhidi ya maambukizi.
Amesema ufuatiliaji wa afya ya mama na mtoto unapaswa kuwa wa karibu na endelevu, kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa, ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa na tija katika kupunguza maambukizi mapya ya VVU.
Aidha, amezitaka FHI 360 na timu za usimamizi wa huduma za afya kuweka nguvu katika upimaji wa VVU wa kimkakati ili kuwabaini watu ambao bado hawajui hali zao za maambukizi na kuwaunganisha na huduma stahiki.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuyafikia makundi yaliyo katika hatari kubwa zaidi ya maambukizi ya VVU kwa kuyapatia huduma rafiki zinazozingatia ridhaa ya mhusika, usiri na miongozo ya kitaifa, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha mradi unaleta matokeo yanayoonekana kwa jamii.
Kikao cha uzinduzi wa mradi huo kimefanyika Oktoba 28, 2026, katika ukumbi wa Hoteli ya Sunset, Iringa, kikihudhuriwa na wawakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, Wizara ya Afya, viongozi wa mkoa na halmashauri, wataalamu wa afya pamoja na wawakilishi wa mashirika yanayoshiriki katika utekelezaji wa mradi huo.
Washiriki wengine ni pamoja na wajumbe wa Timu ya Usimamizi na Uendeshaji wa Huduma za Afya Mkoa (RHMT), wataalamu wa FHI 360 Tanzania, wawakilishi wa JHPIEGO na wataalamu kutoka HUHESO Foundation–Iringa.


.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
TAFUTA HABARI
Kamusi
Social Plugin