Na Dotto Kwilasa ,Dodoma
Wakazi wa Jiji la Dodoma wanakabiliwa na pengo la upatikanaji wa maji safi la lita milioni 68.9 kwa siku, huku Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) ikisema inaendelea na mipango ya kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.
Pengo hilo linatokana na mahitaji ya maji kufikia lita milioni 159.9 kwa siku, wakati uwezo wa DUWASA wa kuzalisha maji ni lita milioni 91 pekee kwa siku.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Oktoba 26, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph, amesema eneo la Makutupora ni chanzo kikuu cha maji kinachochangia sehemu kubwa ya uzalishaji unaohudumia jiji hilo.
Kwa mujibu wa Joseph, Makutupora huzalisha lita milioni 61.5 za maji kwa siku, huku kiasi kingine kikitokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo Nzuguni, Iyumbu, Nala, Ihumwa, Nkuhungu, Miganga, Mkonze na Makulu.
Amesema mamlaka hiyo kwa sasa ina visima 72 vinavyofanya kazi katika maeneo mbalimbali, huku visima 17 vilivyopo Makutupora vikichangia sehemu kubwa ya maji yanayozalishwa.
Hata hivyo ameweka Wazi kuwa uhaba wa vyanzo vya maji ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoipa ugumu DUWASA katika kukidhi mahitaji ya wakazi wa Dodoma, hali inayohitaji hatua za kuongeza uzalishaji kadiri mahitaji yanavyoongezeka.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Joseph amesema DUWASA imeandaa mpango wa miaka mitano wa kuongeza uwezo wa uzalishaji kutoka lita milioni 91 hadi lita milioni 121 kwa siku.
Mpango huo ukitekelezwa, utaongeza uzalishaji kwa lita milioni 30 kwa siku. Hata hivyo, kwa kuzingatia mahitaji ya sasa, bado kutakuwa na pengo la lita milioni 38.9 kwa siku kati ya mahitaji na uzalishaji unaolengwa.
Hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika vyanzo vipya vya maji na miundombinu ya uzalishaji ili kupunguza pengo la upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa wakazi wa Dodoma.




TAFUTA HABARI
Kamusi
Social Plugin