Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MSIGWA: KALAMU ZA WAANDISHI ZINA NGUVU YA KUJENGA AU KUDHOOFISHA NCHI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa.

Na Kadama Malunde - Dodoma

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amewataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kwa uwajibikaji katika kulinda taifa, akisisitiza kuwa taarifa zinazotolewa zina nguvu ya kujenga au kudhoofisha nchi.

Msigwa amesema waandishi wa habari wana wajibu wa kulinda maslahi ya taifa bila kujali tofauti zilizopo, akisisitiza kuwa jukumu hilo linahitaji weledi, uzalendo na kuzingatia maadili ya taaluma.

“Tunayo nchi ya kuilinda kupitia kalamu zetu. Tunaweza kutofautiana kwa namna yoyote ile, lakini tusitofautiane kwenye kulinda nchi yetu kupitia kalamu zetu,” amesema.

Ametoa kauli hiyo Oktoba 31, 2026, jijini Dodoma, wakati wa Mkutano Mkuu na Kongamano la Mwaka la Tathmini ya Huduma za Habari na Mawasiliano Vijijini nchini lililoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini Tanzania (RUJAT).
Katika hatua nyingine, Msigwa amewataka wanahabari kutowaachia wanaharakati jukumu la kuhabarisha umma, akieleza kuwa tofauti na wanaharakati wanaoweza kusimamia ajenda maalumu, waandishi wanapaswa kuzingatia maslahi ya wananchi kwa ujumla bila upendeleo.

Amesema kupungua kwa ushawishi wa vyombo vya habari kwa wananchi kunapaswa kufanyiwa utafiti ili kubaini sababu zinazowafanya wananchi kuelekeza usikivu wao katika makundi mengine, huku akisisitiza umuhimu wa wanahabari kurejesha nafasi yao kwa kuandaa habari zinazogusa maisha ya jamii.
Aidha, ameitaka RUJAT kuimarisha uandishi wa habari za vijijini, akieleza kuwa takribani asilimia 65 ya Watanzania wanaishi vijijini, lakini zaidi ya asilimia 80 ya vyombo vya habari vimejikita mijini kwa mujibu wa takwimu za miaka mitano iliyopita, hali inayochangia changamoto na mahitaji ya wananchi wa vijijini kutopata uwakilishi wa kutosha.

Msigwa pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uchumi wa vyombo vya habari na waandishi ili kulinda uhuru na weledi wa taaluma, huku akieleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta ya habari katika kuimarisha mazingira ya utendaji kazi wa wanahabari nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa RUJAT, Neville Meena, amesema chama hicho kinalenga kuboresha uandishi wa habari za vijijini kwa kuhakikisha waandishi hawaishii kuripoti taarifa za mikutano na matamko ya viongozi, bali wanafanya uchunguzi kubaini namna miradi ya maendeleo na matukio mbalimbali yanavyoathiri maisha ya wananchi.
Mwenyekiti wa RUJAT, Neville Meena

Meena amesema uandishi wa habari za vijijini unapaswa kuwa na sura ya watu kwa kuwapa wananchi nafasi ya kueleza changamoto, mahitaji na mafanikio yao. Ameeleza kuwa chama hicho pia kinahitaji kuwekeza katika mafunzo ya waandishi kuhusu uandishi wa habari za vijijini, matumizi ya teknolojia na akili unde (AI) ili kuongeza ubora wa kazi zao.

Naye Katibu wa RUJAT, Prosper Kwigize, amesema chama hicho kimekua kutoka wanachama waanzilishi 20 mwaka 2020 hadi kufikia wanachama 120, huku kikiwa na maombi zaidi ya 60 kutoka kwa waandishi wengine wanaotaka kujiunga.
Katibu wa RUJAT Prosper Kwigize

Kwigize amesema RUJAT imeweka mikakati ya kujenga uwezo wa wanachama, kuimarisha ushirikiano kati ya waandishi kutoka mikoa mbalimbali na kuhakikisha habari zinazotoka vijijini zinapata nafasi katika majukwaa ya habari. Ameongeza kuwa chama hicho kinapanga kuanzisha tuzo maalumu za uandishi wa habari za vijijini mwaka 2027 kwa ajili ya kutambua waandishi wanaozalisha habari zenye kina na matokeo kwa jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com