Na Sheila Ahmadi, Geita
Wakala wa Vipimo (WMA) umewataka wachimbaji, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini kuhakikisha wanatumia mizani iliyohakikiwa na kuthibitishwa na Wakala huo, ili kuepusha udanganyifu kulinda mapato ya Serikali na kuhakikisha kila mdau anapata haki yake.
Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Mwanza, Karimu Zuberi amesema matumizi ya mizani sahihi ni muhimu katika biashara ya madini kwa kuwa madini kama dhahabu na almasi huuzwa kwa kuzingatia uzito, hivyo hitilafu ndogo katika vipimo inaweza kusababisha hasara kubwa kwa muuzaji na mnunuzi.
Akizungumza katika Maonesho ya Madini yanayoendelea mkoani Geita Meneja Wa wakala wa vipimo kutoka Mkoani Mwanza Karimu Zuberi amesema kwa mujibu wa sheria mizani inayotumika katika biashara inapaswa kuhakikiwa na Wakala wa Vipimo angalau mara moja kwa mwaka ili kuhakikisha inatoa vipimo sahihi.
Vilevile matumizi ya mizani ambayo haijahakikiwa yanaweza kusababisha wizi na udanganyifu katika biashara ya madini, huku akisisitiza kuwa kutumia vipimo visivyokidhi matakwa ya sheria ni kosa linaloweza kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Sababu nyingine ya kutumia mizani iliyohakikiwa ni kuepusha wizi na udanganyifu. Madini kama dhahabu na almasi huuzwa kwa kuzingatia uzito hivyo kama mzani si sahihi, mnunuzi au muuzaji anaweza kupata hasara kubwa,” amesema Meneja Zuberi.
Katika hatua nyingine matumizi ya mizani sahihi yana mchango katika kulinda mapato ya Serikali yanayotokana na madini ikiwemo mrabaha na kodi mbalimbali, kwa kuwa kiwango cha madini kinapaswa kupimwa kwa usahihi kabla ya makato na malipo ya Serikali kufanyika.
Aidha Wakala wa Vipimo Tunahusika na uhakiki wa vipimo mbalimbali vinavyotumika katika shughuli za uchimbaji na biashara, ikiwemo mita za maji, mita za umeme, mizani na mita za kupimia mafuta yanayotumika kwenye mitambo.
Naye Meneja wa Wakala wa Vipimo kutoka Mkoa wa KageraJohnson Japhet ameongeza kuwa wananchi wanaotumia gesi wanapaswa kuhakikisha wanapatiwa gesi kwa kipimo sahihi kwa kutumia mizani iliyohakikiwa.
Hata hivyo Meneja Japhet ameongeza hatua hiyo itasaidia kupunguza malalamiko ya wananchi kuhusu kiwango cha gesi kinachowekwa kwenye mitungi na kuhakikisha mtumiaji analipia kiasi halisi cha bidhaa anachopokea.
“Tunatumia mitungi ya gesi na changamoto imeibuka kuhusu kiwango cha gesi kinachowekwa. Mwananchi anapofika eneo la kuuzia gesi, ahakikishe muuzaji ana mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo ili aweze kupimiwa gesi kwa usahihi,” amesema Meneja Japhet".
wananchi wanapaswa kuwa sehemu ya kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika biashara vinakidhi matakwa ya sheria kwa kuwa matumizi ya vipimo sahihi yanamlinda mtumiaji na mtoa huduma.
Maonesho hayo yameendelea kuwahusisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini na wananchi kutoka Geita na mikoa jirani kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu fursa, huduma na matumizi sahihi ya vipimo katika shughuli za kiuchumi.

Social Plugin