Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PSSSF YAWATAKA WAANDISHI KUWAELIMISHA WANACHAMA KUHAKIKI MICHANGO NA MAFAO KIDIJITALI


Afisa Msimamizi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Mkoa wa Simiyu Salum Mwegelo akizungumza.
Mratibu wa Tanzania Bloggers Network (TBN) Kanda ya Ziwa Kadama Malunde akizungumza kwenye mafunzo hayo kwa niaba ya Mwenyekiti wa (TBN) Beda Msimbe.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga Greyson Kakuru akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Makamu Mwenye wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Simiyu Paschal Michael akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Afisa Uhusiano kutoka PSSSF Abdul Njaidi akizungumza katika mafunzo hayo.

Na Neema Nkumbi - Shinyanga

MFUKO wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umewataka waandishi wa habari kutumia taaluma yao kuwaelimisha na kuwahamasisha wanachama kuhakiki taarifa za michango na mafao yao kupitia mifumo ya kidijitali.

Hatua hiyo imeelezwa kulenga kuhakikisha taarifa zao zinakuwa sahihi na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa kudai mafao.

Wito huo umetolewa leo, Septemba 18, 2026, mjini Shinyanga wakati wa semina ya PSSSF kwa waandishi wa habari kutoka Mtandao wa Wanablogu Tanzania (Tanzania Bloggers Network – TBN) na Klabu za Waandishi wa Habari za mikoa ya Shinyanga na Simiyu.

Katika semina hiyo, Msimamizi PSSSF Mkoa wa Simiyu Salum Miraji ameeleza kuwa matumizi ya mifumo ya kidijitali yamekuwa sehemu ya maboresho ya huduma za mfuko, yakilenga kumwezesha mwanachama kupata na kuhakiki taarifa zake bila kulazimika kufika katika ofisi za PSSSF.

Ameeleza kuwa mwanachama anaweza kutumia mfumo huo kufuatilia taarifa zake, ikiwemo taarifa za michango, na kubaini mapema endapo kuna taarifa zisizo sahihi ambazo zinaweza kuleta changamoto wakati wa uchakataji wa mafao.
PSSSF imewataka waandishi wa habari kutumia majukwaa yao kuwaelimisha wanachama kuhusu umuhimu wa kufanya uhakiki huo mapema, badala ya kusubiri hadi wanapofikia hatua ya kustaafu au kuhitaji mafao.

Katika semina hiyo, Mratibu wa Tanzania Bloggers Network – TBN Kanda ya Ziwa, Kadama Malunde, amesisitiza umuhimu wa waandishi kutumia nafasi yao na taaluma waliyonayo kuwafikishia wananchi elimu na taarifa sahihi zinazoweza kuwasaidia kutambua haki na huduma wanazostahili.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, Malunde amesema waandishi wana nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanaelewa masuala ya hifadhi ya jamii, ikiwemo umuhimu wa wanachama kufuatilia taarifa zao za michango na mafao kwa kutumia mifumo inayotolewa na taasisi husika.
Amesema mafunzo wanayopata waandishi yanapaswa kuwa chachu ya kuongeza uelewa wao na baadaye kutumia ujuzi huo kuwaelimisha wananchi kwa lugha rahisi, sahihi na inayoeleweka.

“Leo tunapaswa kuwa na furaha ya kupata elimu. Kwa mwandishi wa habari, kujifunza ni sehemu ya kazi yetu. Dunia inabadilika, teknolojia inabadilika na mahitaji ya jamii yanabadilika,” amesema Malunde.

Malunde amesema TBN, iliyoanzishwa mwaka 2015, imeendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali, ikiwemo PSSSF, katika mafunzo na ujenzi wa uwezo wa wanablogu na watengeneza maudhui nchini.

Amesema maendeleo ya teknolojia yameongeza kasi ya usambazaji wa taarifa, hivyo waandishi wanapaswa kuwa makini kuhakikisha taarifa wanazozifikisha kwa jamii zinathibitishwa, zina usahihi na zinazingatia misingi ya uwajibikaji wa taaluma.
“Taarifa za kidijitali zinaweza kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi. Hivyo, nidhamu, usahihi na uwajibikaji ni muhimu sana. Uwezo wetu na nidhamu yetu ndiyo misingi inayoweza kutufanya kuwa waandishi bora na wenye mchango mkubwa kwa jamii,” amesema.

Aidha, Malunde amesema historia ya TBN inaonesha umuhimu wa kujifunza, kushirikiana na kujenga uwezo miongoni mwa waandishi na watengeneza maudhui ili kuongeza mchango wao katika jamii.

“Tanzania ina waandishi wenye uwezo mkubwa, na tunapaswa kuendelea kuutumia uwezo huo kwa manufaa ya jamii. Tuyatumie mafunzo haya kupata uelewa zaidi na kisha kuwafikishia wananchi taarifa kwa lugha rahisi na inayoeleweka,” amesema.

Amesisitiza kuwa mwandishi wa habari ana wajibu wa kuthibitisha taarifa kabla ya kuzichapisha au kuzitangaza, kuheshimu vyanzo vya habari na kuwajibika kwa maudhui anayoyafikisha kwa umma.

“Mwandishi wa habari anatakiwa kuthibitisha taarifa, kuheshimu vyanzo vya habari na kuwajibika kwa kila anachochapisha au kukitangaza,” ameongeza.
Naye Kaimu Afisa Mfawidhi PSSSF Shinyanga Sunday Rashid amesema mfuko huo umeendelea kuboresha mchakato wa maandalizi ya mafao kwa kuanza kushughulikia taarifa za mtumishi anayekaribia kustaafu miezi sita kabla ya tarehe yake rasmi ya kustaafu.

Hatua hiyo inalenga kutoa muda wa kutosha wa kuhakiki taarifa za mwanachama na kushughulikia changamoto zinazoweza kujitokeza kabla ya kufikia muda wa kustaafu.

Semina hiyo imelenga kuwajengea waandishi uelewa kuhusu huduma za PSSSF ili waweze kutumia taaluma yao kuelimisha jamii, hususan wanachama, kuhusu haki, wajibu na namna ya kufuatilia taarifa zao za hifadhi ya jamii.

TAZAMA PICHA NA MARCO MADUHU👇👇
Afisa Msimamizi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Mkoa wa Simiyu Salum Mwegelo akizungumza.
Afisa Uhusiano kutoka PSSSF Abdul Njaidi akizungumza katika mafunzo hayo.
Afisa Mahusiano na Mtoa elimu kwa wanachama PSSSF Flora Sumari, akizungumza katika mafumo hayo.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga Greyson Kakuru akizungumza kwenye mafunzo hayo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com