Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ALIYEWANIA UBUNGE SHINYANGA ATWAA TAJI LA MISS UNIVERSE TANZANIA 2026


Na Michael Abel, Shinyanga.

Elizabeth Makune kutoka Jijini Mwanza ametangazwa kuwa mshindi wa Miss Universe Tanzania 2026, baada ya kuibuka kidedea katika fainali ya mashindano hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia Septemba 21, 2026.

Kwa ushindi huo, Makune amejinyakulia taji la Miss Universe Tanzania 2026 pamoja na zawadi ya Sh milioni 20. Ushindi huo pia umempa nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss Universe ya Dunia, ambako atabeba jukumu la kuiwakilisha nchi katika jukwaa la kimataifa.

Katika fainali hiyo, Sandra Giovina alimaliza katika nafasi ya pili na kujishindia zawadi ya Sh milioni 10, huku washiriki wengine wakipata nafasi na zawadi mbalimbali. Mashindano hayo yaliandaliwa na Millen Privé & Co. Lifestyle.

Ushindi wa Miss Universe Tanzania 2026 unaongeza sura nyingine katika historia ya Elizabeth Makune katika mashindano ya urembo. Makune aliwahi kutwaa taji la Miss Tanzania 2018 akiwa na umri wa miaka 22 na baadaye kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss World 2018 yaliyofanyika nchini China.

Kabla ya kutwaa taji la Miss Tanzania, Makune alikuwa tayari amejijengea jina katika mashindano ya kimataifa baada ya kushinda Miss World University Africa 2017, shindano lililowakutanisha washiriki kutoka mataifa 53 ya Afrika na kufanyika nchini Korea Kusini.

Kwa mujibu wa wasifu wake wa Miss World, Makune ana shahada ya Public Sector Accounting and Finance na ameendelea na masomo ya juu. Pia amewahi kujihusisha na shughuli mbalimbali nje ya ulimwengu wa mashindano ya urembo, zikiwemo biashara, kilimo na utalii wa ndani kupitia mpango wa Twenzetu Kutalii pamoja na kushiriki kuwania nafasi mbalimbali kwenye siasa.

Katika siasa Miss Makune mnamo 2024 aliwania ridhaa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kugombea Ubunge wa EALA lakini hakuchaguliwa, 2025 Aliwania Ubunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga kupitia CCM na kufanikiwa kupata kura 19 katika kura za maoni lakini Hakufanikiwa kuingia katika nafasi mbili za juu zilizokwenda kwa Santiel Kirumba na Dkt. Christina Mnzava.

Kwa sasa, ushindi wa Miss Universe Tanzania 2026 unamrudisha Makune kwenye jukwaa la mashindano ya urembo baada ya miaka kadhaa tangu kutwaa Miss Tanzania 2018. Safari yake mpya inalenga kumpeleka katika hatua ya kimataifa akiwa mwakilishi wa Tanzania katika Miss Universe, huku akiwa na uzoefu wa awali wa kuiwakilisha nchi katika mashindano makubwa ya kimataifa.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com