Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

GST YATOA ELIMU YA UTAFITI WA KIJIOLOJIA KWA WANANCHI



Na Sheila Ahmadi, Geita

Taasisi ya Jiolojia Tanzania (GST) imeendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau wa sekta ya madini kuhusu tafiti za kijiolojia pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo, kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Madini na Teknolojia yanayoendelea mkoani Geita.

Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Masoko wa GST, Jeremiah Mgare, alisema taasisi hiyo ambayo ipo chini ya Wizara ya Madini imeshiriki maonesho hayo kwa lengo la kuwafikia wananchi na kuwaeleza huduma zinazotolewa pamoja na matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanywa nchini.

Amesema Wananchi wanaotembelea banda la GST wanapata fursa ya kukutana na wataalamu mbalimbali, wakiwemo wataalamu wa maabara, ambao hutoa elimu na ushauri kuhusu masuala ya utafiti wa madini na jiolojia.

“Katika banda letu, Wananchi watapata huduma mbalimbali zikiwemo ushauri elekezi, pamoja na fursa ya kukutana na wataalamu wetu ambao watatoa elimu kuhusu tafiti za madini na masuala ya kijiolojia,” amesema Mgare.

Kwa upande wake Mjiolijia kutoka Taasisi ya utafiti wa madini GST Andrew Buluba amesema kuwa GST imefanya tafiti mbalimbali nchini, zikiwemo tafiti za jiolojia, jiokemia na jiofizikia, ambazo zimekuwa muhimu katika kutambua na kuelewa rasilimali za madini zilizopo katika maeneo mbalimbali.

Kwa mujibu wa Buluba, tafiti zilizofanywa na taasisi hiyo zinajumuisha utafiti wa jiokemia kwa kiwango cha asilimia 24, tafiti za jiolojia kwa asilimia 98, pamoja na tafiti za jiofizikia kwa kutumia teknolojia mbalimbali.

Aidha, amesema GST pia inahusika na kuratibu na kutoa ushauri kuhusu majanga asilia, yakiwemo maporomoko ya ardhi, huku ikitoa elimu kwa wananchi kuhusu namna bora ya kujikinga na athari zinazoweza kusababishwa na majanga hayo.

Buluba amewataka wananchi na wadau wa sekta ya madini kutumia fursa ya maonesho hayo kutembelea banda la GST ili kupata elimu kuhusu tafiti zilizofanywa na taasisi hiyo pamoja na huduma zinazotolewa.

“Tunawakaribisha wananchi wote kutembelea banda letu ili kujifunza mambo mbalimbali yanayohusiana na shughuli za GST na kuona tafiti mbalimbali ambazo taasisi imewahi kufanya,” amesema Buluba.

Aliongeza kuwa maonesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kuona kwa vitendo baadhi ya kazi na matokeo ya tafiti zilizofanywa na GST na kuelewa namna taarifa za kijiolojia zinavyoweza kusaidia katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com