Na Sheila Ahmadi, Dodoma
Waandishi wa habari nchini wameanza kuonyesha kwa vitendo umuhimu wa matumizi ya bima, baada ya waandishi 11 kuchukua bima za maisha na mali ndani ya siku moja katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni ishara ya kuongezeka kwa uelewa miongoni mwa waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa bima katika kulinda maisha, familia na mali dhidi ya majanga yasiyotarajiwa.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa Maonesho ya Nanenane, Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa Shirika la Bima la Taifa (NIC Insurance), Karimu Meshack, amesema hatua ya waandishi hao kuchukua bima ina umuhimu mkubwa kwa kuwa wao ni miongoni mwa wadau wanaohamasisha jamii kutumia huduma hiyo.
Meshack amesema waandishi wa habari wamekuwa wakitoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa bima, hivyo uamuzi wao wa kuchukua bima unadhihirisha kuwa wameanza kutekeleza kwa vitendo ujumbe wanaoufikisha kwa wananchi.
“Waandishi wa habari ni daraja muhimu la kuwafikishia wananchi elimu ya bima. Wanapochukua bima wao wenyewe, wanakuwa mfano wa kuigwa na jamii na pia wanapata uzoefu wa moja kwa moja wa umuhimu wa huduma hiyo,” amesema Meshack.
Amesema waandishi wa habari, kama ilivyo kwa wananchi wengine, wanakabiliwa na majukumu ya kifamilia na changamoto mbalimbali za maisha, hivyo wanahitaji kuwa na ulinzi wa kifedha unaoweza kuwasaidia kukabiliana na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na majanga.
Kwa upande wake, mwandishi wa habari, Sophia Kingimali, amesema wamechukua hatua hiyo kwa lengo la kulinda maisha yao, familia pamoja na mali walizowekeza.
Aidha, amesema bima ya maisha inaweza kusaidia familia kupata ulinzi wa kifedha endapo yatatokea majanga yasiyotarajiwa, huku bima ya mali ikiwa muhimu katika kulinda vitega uchumi dhidi ya hasara zinazoweza kusababishwa na majanga mbalimbali.
Vilevile, Meshack amewahimiza waandishi wengine nchini pamoja na wananchi kwa ujumla kutumia fursa zinazopatikana katika Maonesho ya Nanenane kupata elimu na kuchagua huduma za bima zinazoendana na mahitaji yao.
Amesema kuongezeka kwa matumizi ya bima kutasaidia kujenga jamii yenye uelewa na utamaduni wa kujikinga na majanga, huku ikichangia kuimarisha usalama wa kifedha wa familia na uchumi wa taifa.

Social Plugin