Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC MASINDI APONGEZA HATUA ZA MLEZI WA KISHAPU VETERAN

Na Sumai Salum – Kishapu

Timu ya Kishapu Veteran wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga, imepata hamasa mpya baada ya mlezi wake, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Malipo wa CRDB Bank, kukabidhi jezi za mazoezi kwa timu hiyo, huku akianza na mpango wa kuhakikisha uongozi wa timu unaanzisha mchakato wa kupata uwanja wao wa michezo.

Akizungumza Agosti 6, 2026 alipokutana na timu hiyo kwa mara ya kwanza na kujitambulisha baada ya kupokea uteuzi wa kuwa mlezi wa Kishapu Veteran, Chabba amesema jambo kubwa aliloanza nalo ni kuutaka uongozi wa timu kuanza mara moja mchakato wa kutafuta na kupata eneo litakalotumika kama uwanja wa michezo wa timu hiyo, akieleza kuwa uwepo wa uwanja ni msingi muhimu wa kuendeleza mazoezi, vipaji na michezo kwa ujumla.

Chabba amesema hataki nafasi yake ya ulezi iishie katika kukabidhi jezi na vifaa vya michezo pekee, bali anataka kuona kuna mipango ya muda mrefu itakayoiwezesha Kishapu Veteran kuwa na mazingira yake bora ya kufanya mazoezi na kuendesha shughuli mbalimbali za michezo.

Amesema uwanja huo unaweza kuwa sehemu muhimu ya kuunganisha wanamichezo, jamii na wadau mbalimbali, huku ukiwa fursa ya kuandaa shughuli za michezo zitakazoweza kusaidia timu kupata vyanzo vya mapato na kujenga uwezo wa kujiendesha.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, amempongeza Chabba kwa kukubali kuwa mlezi wa Kishapu Veteran na kuanza na wazo la msingi la kuhakikisha timu inapata uwanja wake wa michezo.
Mkuu wa kitengo cha malipo Benki ya CRDB ambaye pia ni Mlezi wa timu ya Kishapu Veteran Madaha Chabba akizungumza wakati wa hafla ya kuzungumza na wachezaji na viongozi wa timu hiyo na kisha kukabidhi jezi za mazoezi zilizotolewa na benki hiyo Agosti 5, 2026 wilayani Kishapu mkoani Shinyanga

Mhe. Masindi pia amempongeza Mkurugenzi wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, akimtaja kuwa ni kiongozi anayeunga jitihada za Mhe. Rais Samia Suluhu za kupenda michezo na kutoa nafasi kwa shughuli za michezo katika jamii. Amesema ushirikiano huo ni fursa ambayo Kishapu inapaswa kuitumia vizuri katika kukuza michezo na kuibua fursa za kiuchumi.

“Tunampongeza sana mlezi wetu kwa kuanza na jambo kubwa la kutafuta uwanja wa Kishapu Veteran. Jezi ni muhimu, mipira ni muhimu, lakini kuwa na uwanja wa kudumu ni msingi wa maendeleo ya timu. Tunataka uongozi uanze mchakato huo na wadau tushirikiane kuhakikisha tunafikia lengo hilo,” amesema Mhe. Masindi.

Amesema uongozi wa Kishapu Veteran unatakiwa kutumia nafasi hiyo kujenga mipango ya muda mrefu, ikiwemo namna ya kutengeneza fedha na kujiendesha kwa kujitegemea, badala ya kutegemea misaada pekee huku wakiendelea kuwa bora katika kuleta udshindi wa michezo mbalimbali watakayocheza ili kuwatia moyo wananchi na hata mlezi wa timu hiyo.

Masindi ameongeza kuwa lengo lao ni kuhakikisha jina Kishapu Veteran linakuwa na maana ya michezo, nidhamu, ushindani na mafanikio, akiwataka wachezaji kujituma katika mazoezi na kutumia fursa hiyo kuleta matokeo yatakayowafanya wadau wa timu kujivunia mchango wao.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhiwa jezi za mazoezi kwa timu ya mpira wa miguu ya kishapu veteran kutoka Benki ya CRDB zikikabidhiwa na mlezi wa timu hiyo Madaha Chabba wilayani humo Agosti 6, 2026

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kishapu Veteran Sostenes Amasi amemshukuru mlezi Chabba kwa kukubali kuwa sehemu ya familia ya timu hiyo, akisema uteuzi wake umeleta nguvu mpya na mawazo mapya yenye kulenga maendeleo ya timu.


“Tunamshukuru sana mlezi wetu kwa kukubali kutusimamia. Jambo la kwanza alilotuambia ni kwamba hataki tuishie kwenye jezi, bali tuanze mchakato wa kupata uwanja wetu. Hili ni jambo kubwa sana kwetu kwa sababu uwanja utakuwa urithi wa timu na jamii ya Kishapu kwa ujumla, Mkuu wetu wa Wilaya pia tunampongeza kwa kuendelea kuwa mshauri na msimamizi wetu kila mara tunapomhitaji anakuwepo kwa hali na mali kwa ajili yetu hawa ni viongozi wa mfano,” amesema Mwenyekiti huyo.


Amesema uongozi wa timu uko tayari kushirikiana na mlezi, Serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha mchakato wa kupata uwanja unafanikiwa, huku ukiendelea kusimamia mazoezi, nidhamu na ushindani wa timu.

Hatua ya mlezi huyo kuanza na mpango wa kupata uwanja imeonekana kuwa muhimu zaidi kuliko msaada wa vifaa pekee, kwani ikifanikiwa inaweza kuipa Kishapu Veteran msingi wa kudumu wa kufanya mazoezi, kuandaa mashindano na hata kujenga chanzo cha mapato kwa timu na jamii.
Mwenyekiti wa Kishapu Veteran iliyoko wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Sostenes Amasi. (aliyevalia Tisheti yenye rangi nyekundu)








































Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com