Na Sheila Ahmadi, Dodoma
Jumuiya ya Wakulima wa Parachichi Tanzania (ASTA) imewataka wakulima kutumia Maonesho ya Nanenane kama jukwaa la kupata elimu, taarifa na fursa zinazoweza kuwawezesha kuongeza uzalishaji, ubora na ushindani wa zao la parachichi katika masoko.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mkuu wa Jumuiya hiyo, Eli Ongori, amesema kuwa jumuiya hiyo yenye wanachama wapatao 550 kutoka katika mikoa inayolima parachichi nchini, imekuwa ikiunganisha wakulima na wadau kutoka sehemu mbalimbali wa sekta ya kilimo, ikiwemo AGCOT, katika kutafuta fursa na suluhisho za changamoto zinazowakabili.
Kupitia ushirikiano huo ni muhimu kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wakulima wanaojihusisha na kilimo cha parachichi, jambo ambalo limeibua changamoto katika maeneo mbalimbali, ikiwemo ubora wa mazao upatikanaji wa masoko pembejeo na mitaji.
“Lengo kubwa la jumuiya ni kutetea maslahi ya wakulima wa parachichi katika kuhakikisha wakulima wanapata elimu na mafunzo ya kilimo bora, masoko ya uhakika, pembejeo bora kwa gharama nafuu pamoja na mitaji yenye masharti rafiki,” amesema Ongori.
Aidha kupitia ushirikiano na taasisi za Serikali pamoja na wadau wa sekta ya kilimo kama AGCOT, wakulima wanaweza kupata fursa za kujengewa uwezo, kuunganishwa na wadau wa mnyororo wa thamani na kupata taarifa muhimu zitakazowasaidia kuongeza tija katika uzalishaji.
Sanjari na hayo Ongori ameongeza kuwa jumuiya hiyo pia inalenga kujenga jukwaa litakalowawezesha wakulima wa parachichi kuwa na sauti ya pamoja katika ngazi mbalimbali, ikiwemo Serikali, ili changamoto zinazowakabili ziweze kufikishwa na kutafutiwa ufumbuzi.
Kupitia Maonesho Hayo ya Nanenane ni fursa muhimu kwa wakulima kukutana na wadau mbalimbali na kupata taarifa kuhusu maendeleo ya zao la parachichi, ikiwemo masoko, teknolojia za uzalishaji na fursa za uwekezaji.
“Tunawakaribisha wakulima wa parachichi wanaofika Nanenane wapite katika banda letu ili kupata taarifa mpya kuhusu kinachoendelea katika zao hili, ikiwemo taarifa kutoka Wizara ya Kilimo na taasisi mbalimbali tunazoshirikiana nazo,” amesema.
Ameongeza kuwa taarifa na elimu wanazopata wakulima kupitia majukwaa hayo zitawasaidia kufanya maamuzi sahihi katika uzalishaji na biashara ya parachichi, huku akisisitiza umuhimu wa wakulima kutumia fursa zinazopatikana kupitia Nanenane na wadau wa sekta ya kilimo.
Katika Hatua nyingine Wakulima wataweza kuongeza ubora wa mazao, tija na ushindani wa parachichi la Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Social Plugin