Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI SANGU: BONDE LA ZIWA RUKWA NI HAZINA YA AJIRA KWA VIJANA

Mbunge wa Jimbo la Kwela ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Deus Sangu akipata Maelezo kutoka kwa msimamizi wa mradi wa ujenzi wa madarasa Noble Helium ambayo Inafanya shughuli za utafiti na uchimbaji wa gesi ya helium Christian Temba (20 Julai 2026) alipokuwa akikagua miradi ya Maendeleo katika Kijiji cha Kinambo Kata ya Milepa Wilaya ya Sumbawanga.
Mbunge wa Jimbo la Kwela na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi,Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lwanji Tarafa ya Kipeta Sumbawanga ambapo amewasihi kuendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo jana. Kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Ephraim Konta

( Picha na OWM- KAM)

*****************


Na: OWM (KAM), Sumbawanga

Mbunge wa Jimbo la Kwela ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Deus Sangu amewataka vijana wa Mkoa wa Rukwa kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa za ajira zinazozalishwa na mradi wa kimkakati wa uchimbaji wa gesi ya helium katika Bonde la Ziwa Rukwa.

Sangu alitoa wito huo Julai 20, 2026 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kinambo Kata ya Milepa Wilaya ya Sumbawanga akisema mradi huo una nafasi kubwa ya kuongeza ajira na kuinua uchumi wa wananchi hususan vijana wa maeneo yanayouzunguka.

Alisema Serikali imeingia makubaliano na kampuni ya Marekani ya Noble Helium kufanya shughuli za utafiti na uchimbaji wa gesi ya helium katika ukanda wa Bonde la Ziwa Rukwa, ambapo shughuli hizo tayari zimeanza na kuendelea kuzalisha nafasi mbalimbali za ajira.

Waziri Sangu ambaye ndiye mwenye dhamana na masuala ya ajira nchini alisema tayari amefanya mazungumzo na viongozi wa kampuni hiyo ili kuhakikisha vijana wa Kijiji cha Kinambo kilicho jirani na mradi huo wa gesi na Mkoa wa Rukwa wanapewa kipaumbele katika nafasi za ajira zinazopatikana kupitia mradi huo.

“Fursa za ajira katika mradi huu ni nyingi. Lengo letu ni kuona vijana wa maeneo haya wananufaika moja kwa moja kwa kupata ajira zitakazowaongezea kipato na kuboresha maisha yao,” alisema.

Mbali na kutoa ajira kampuni ya Noble Helium imeanza kutekeleza shughuli za uwajibikaji kwa jamii kwa kujenga madarasa mawili katika Shule ya Msingi Kinambo hatua inayolenga kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto wa eneo hilo.

Akizungumza kwa niaba ya kampuni hiyo msimamizi wa mradi wa ujenzi wa madarasa Christian Temba alisema ujenzi huo ni sehemu ya mchango wa kampuni katika kuunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanywa na wananchi na Serikali katika sekta ya elimu.

Katika ziara hiyo Sangu pia alikabidhi madawati 20 kwa Shule ya Msingi Msia iliyopo Kata ya Milepa. Madawati hayo yametolewa kwa ufadhili wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na yanatarajiwa kunufaisha wanafunzi zaidi ya 60 kwa kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Aidha, aliwahakikishia wananchi wa Jimbo la Kwela kuwa ataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutafuta misaada na rasilimali za kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa utekelezaji wa ahadi zake za uchaguzi wa mwaka 2025 unaendelea kwa vitendo.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Ephraim Konta, alimpongeza Waziri Sangu kwa mchango wake katika miradi ya maendeleo akisema msaada wake wa vifaa vya ujenzi umechangia kukamilika kwa ujenzi wa madarasa katika Shule za Msingi Lwanji na Kanyala hatua iliyotoa unafuu kwa wananchi wengi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com