Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHEREHE ZA SIKU YA KISWAHILI DUNIANI ZAFANA NCHINI ALGERIA

Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, amesema lugha ya Kiswahili inaendelea kukua na kuenea duniani ambapo sasa inazungumzwa na watu zaidi ya milioni 200 katika nchi 14 duniani na kutumika rasmi katika jumuiya kadhaa za kikanda barani Afrika na kimataifa.

Balozi Matinyi aliyasema hayo kwenye sherehe za Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani zilizoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Algeria na kufanyika jijini Algiers tarehe 9 Julai zikihudhuriwa na mabalozi, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, taasisi za umma na binafsi, wanazuoni na waandishi wa habari walioongozwa na Katibu Mnadhimu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni na Sanaa ya Algeria, Bibi Nacera Ayaïchia.

“Mbali ya Tanzania, Kiswahili pia ni lugha ya taifa nchini Kenya, Uganda, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),” alisema Balozi Matinyi kwenye hotuba yake aliyoitoa kwa lugha ya Kiswahili na nakala yake katika tafsiri ya lugha za Kiarabu, Kifaransa na Kiingereza kusambazwa kwa wageni waalikwa waliopewa fursa ya kuifuatilia kwa sauti na maandishi kwenye skrini kubwa.

Sherehe hiyo ilinogeshwa na filamu fupi ya dakika kumi iliyoonesha marais wa zamani na wa sasa wa Tanzania na baadhi wa nchi za mashariki, kati na kusini mwa Afrika wakihutubia kwa lugha ya Kiswahili katika nyakati tofauti.

Filamu hiyo pia inamuonesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akihutubia kwa lugha ya Kiswahili nchini Komoro mwaka 2025 kwenye sherehe za miaka 50 ya uhuru wa taifa hilo.

Balozi Matinyi aliongeza pia kwamba Kiswahili ni lugha rasmi ya Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Kadhalika, Balozi Matinyi aliitaja mifano ya redio za nchi za Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Japan, China, Iran, India na wakati fulani Marekani ambazo hutumia lugha ya Kiswahili katika matangazo yake ya kila siku.

Akirejea kauli mbiu ya mwaka huu ya siku hiyo ya “Kiswahili kwa Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Uchumi Duniani”, Balozi Matinyi alisema Kiswahili ni lugha ya kujivunia ambayo imetumika katika mapambano ya ukombozi barani Afrika na inaendelea kutumika kulinda amani, kuleta mshikamano na kujenga uchumi barani Afrika.

Sherehe hiyo iliyotumia lugha nne zikiongozwa na Kiswahili, ilipambwa pia na vinywaji vya chai na kahawa ya Tanzania, vyakula vya mapishi ya Kiswahili, maonesho ya mavazi ya wakaazi wa Pwani ya Tanzania kama khanga, baibui, kanzu, vikoi na vitenge yaliyooneshwa na wanafunzi wa Tanzania.

Wanafunzi hao wa Tanzania wanaosoma kwenye vyuo vikuu nchini Algeria, walicheza pia ngoma mbili za makabila ya Tanzania ya Kimasai na Kihaya na kuimba shairi la Kiswahili.


Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani huadhimishwa mwezi Julai tangu mwaka 2022 kufuatia uamuzi wa UNESCO wa mwaka 2021 wa kuitangaza tarehe 7 Julai kuwa siku ya maadhimisho ya lugha hii pekee barani Afrika kuwahi kupewa hadhi hii kimataifa.

Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania
Algiers, Julai 10, 2026.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com