Kombe la ubingwa wa Klabu ya Yanga Afrika linalotarajiwa kuwasili mkoani Ruvuma tarehe 25 julai 2026 kwaajili ya sherehe kubwa ya kusherehekea ubingwa wa Klabu hiyo mara tano mfululizo huku mgeni rasmi akiwa mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed
Katibu wa chama cha Mapinduzi CCM wilaya James Mgego akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama wilaya Songea ujio wa kombe la ubingwa wa Klabu ya Yanga Afrika tarehe 25 julai 2026Na Regina Ndumbaro -Songea-Ruvuma
Mkoa wa Ruvuma unatarajia kuandika historia Julai 25, 2026 kwa kuandaa sherehe kubwa za kusherehekea ubingwa wa Klabu ya Yanga Afrika baada ya kutwaa taji la ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara kwa mara ya tano mfululizo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea, James Mgego, amesema tukio hilo litafanyika mjini Songea na mgeni rasmi atakuwa mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, ambaye amemtaja kuwa mwanamichezo namba moja na mwanachama wa muda mrefu wa Yanga.
Amesema ujio wa kombe hilo mkoani Ruvuma ni tukio la kihistoria litakalowakutanisha mashabiki wa soka na wananchi kutoka maeneo mbalimbali.
Mgego amesema shughuli za siku hiyo zitaanza asubuhi kwa dua na sala maalumu za kuiombea klabu ya Yanga, ikiwa ni pamoja na kuwaombea majeruhi wa timu akiwemo Pacome, pamoja na kuliombea zoezi la uchaguzi wa viongozi wa klabu.
Baada ya hapo kutakuwa na chakula cha pamoja na wazee wa mji, huku kombe la ubingwa likitarajiwa kuwasili mapema kabla ya kuzungushwa katika mitaa na maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Songea ili wananchi wapate fursa ya kuliona na kushiriki katika shamrashamra za ushindi huo.
Aidha, amesema shughuli zitahitimishwa kwa burudani kubwa ya jioni iliyopewa jina la "Usiku wa Mabingwa", ambapo kutakuwa na muziki, vyakula, vinywaji na nyama choma.
Amesema tiketi za kushiriki zinapatikana katika ofisi za chama na maeneo mbalimbali ya Songea kwa bei ya shilingi 30,000 kwa tiketi ya mtu mmoja na shilingi 50,000 kwa tiketi ya watu wawili.
Mgego amewaalika mashabiki wote wa soka, wakiwemo wasiokuwa wanachama wa Yanga na hata mashabiki wa timu pinzani, kujitokeza kushuhudia kombe hilo na kushiriki katika sherehe hizo za kihistoria.
Mgego pia amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, kwa mchango wake katika kuhamasisha michezo mkoani humo, pamoja na kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuendeleza sekta ya michezo nchini.
Amesema katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, klabu za Tanzania zimeendelea kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa kupitia hamasa ya "Goli la Mama".
Aidha, amesisitiza kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kuimarisha umoja, amani, mshikamano na ajira kwa vijana, na kwamba maendeleo hayo yanaendana na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inayotambua michezo kama sehemu muhimu ya maendeleo ya taifa.
Social Plugin