Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana dhamira ya dhati ya kuhakikisha Katiba mpya inapatikana na ndio maana suala hilo limewekwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM pamoja na kuahidi kulitekeleza.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa 15 wa wanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) uliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam, akisema suala hilo limejadiliwa tangu mwaka 1992 mara baada ya kuanza kwa vyama vingi, lakini Serikali ya Awamu ya Sita imeahidi kulitekeleza kwa manufaa ya wananchi, akiwasihi wananchi kuibeba ajenda hiyo kwa uzito mkubwa ili iweze kutekelezwa katika kipindi hiki.
"Ili uwe na hakika ya kupata Katiba mpya moja ya jambo la muhimu sana ni utashi wa kupata katiba wa Rais aliyepo madarakani na niwaambie kwa mujibu wa Katiba yetu, Rais anapokaa kwenye kikao cha baraza la Mawaziri, baraza haliamua linashauri, Mawaziri wanashauri, Rais anaamua, akisema hii haitaingia miaka 100 haitaingia."
"Nilipokuwa Katibu Mkuu wa Chama wakati nasimamia uandishi wa Ilani, Kamati ya Ilani ilisema Watanzania wanatamani Katiba mpya, wakaja kuniambia, nikamwambia Mwenyekiti kuwa jambo lenyewe zuri lakini sasa hivi tuna mgombea wa Urais na ni vizuri atuhakikishie kuwa jambo hilo litatelekezwa.
Nikaenda kwa Mwenyekiti nikamueleza, nikamuuliza una utashi jambo hili liingie kwenye Ilani? Akaniambia kwamba hawezi kuacha ahadi yake kama alivyoiahidi Tume ya haki jinai aliyokuwa ameiunda, akasema tuliweke." Amesema Dkt. Nchimbi.
Aidha, Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuzingatia suala la haki, kwani ndio msingi wa amani katika Taifa lolote lile, akibainisha kuwa Serikali itaendelea na wajibu wa kuhakikisha wananchi wanaishi kwa usalama bila hofu.


Social Plugin