
Mratibu wa Tamasha la Utamaduni wa Msukuma, Peter Frank Lugumi maarufu kama Mr. Black, akifanyiwa taratibu za kimila wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni wa Msukuma msimu wa tano, linalofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Nhelegani, Manispaa ya Shinyanga.
Chifu wa Kizumbi Kidola wa Pili, Charles Njange, akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Tamasha la Utamaduni wa Msukuma msimu wa tano lililofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Nhelegani, Manispaa ya Shinyanga, Julai 24, 2026.
Chifu wa Kizumbi Kidola wa Pili, Charles Njange (kushoto mwenye shati la kitenge), akibariki ngoma za asili wakati wa uzinduzi rasmi wa Tamasha la Utamaduni wa Msukuma msimu wa tano lililofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Nhelegani, Manispaa ya Shinyanga, Julai 24, 2026.
Chifu wa Kizumbi Kidola wa Pili, Charles Njange (katikati), akiwasili katika Viwanja vya Shule ya Msingi Nhelegani, Manispaa ya Shinyanga, kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa Tamasha la Utamaduni wa Msukuma msimu wa tano lililoanza Julai 24, 2026.

Mratibu wa Tamasha la Utamaduni wa Msukuma, Peter Frank Lugumi maarufu kama Mr. Black, akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Tamasha la Utamaduni wa Msukuma msimu wa tano katika Viwanja vya Shule ya Msingi Nhelegani, Manispaa ya Shinyanga, Julai 24, 2026.

Mratibu wa Tamasha la Utamaduni wa Msukuma, Peter Frank Lugumi maarufu kama Mr. Black, akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Tamasha la Utamaduni wa Msukuma msimu wa tano katika Viwanja vya Shule ya Msingi Nhelegani, Manispaa ya Shinyanga, Julai 24, 2026.
Mdau wa utamaduni kutoka Nairobi, Kenya, Dominic Mkami wa kabila la Wakamba, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni wa Msukuma msimu wa tano katika Viwanja vya Shule ya Msingi Nhelegani, Shinyanga.
Na Elizabeth Cosmas - Malunde 1 blog Shinyanga
Tamasha la Utamaduni wa Msukuma msimu wa tano, “Shinyanga Sukuma Festival & Business Expo”, limezinduliwa rasmi leo, Julai 24, 2026, katika Viwanja vya Shule ya Msingi Nhelegani, Manispaa ya Shinyanga.
Tamasha hilo limezinduliwa na Chifu wa Kizumbi Kidola wa Pili, Charles Njange, likiwa na lengo la kuenzi, kuhifadhi na kuendeleza urithi wa utamaduni wa Wasukuma kupitia ngoma za asili, maonesho ya biashara, michezo ya watoto pamoja na shughuli mbalimbali za kijamii.
Tamasha hilo litakalofanyika kwa siku tatu kuanzia Julai 24 hadi 26, 2026, limewakutanisha wadau wa utamaduni kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania, likiwa jukwaa la kujifunza mila na desturi za Wasukuma, kukuza vipaji na kutoa fursa za kiuchumi kupitia maonesho ya biashara na bidhaa mbalimbali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Chifu wa Kizumbi Kidola wa Pili, Charles Njange, amesema tamasha hilo ni ishara ya umoja, mshikamano na amani ambayo imekuwa msingi wa Taifa la Tanzania kwa miaka mingi.
Amesema amani ndiyo nguzo muhimu inayowapa wananchi nafasi ya kusherehekea na kuendeleza tamaduni zao, kutambua historia yao, walikotoka, walipo sasa pamoja na mwelekeo wa maisha yao ya baadaye.
“Nawashukuru wananchi wote kwa kufika kwenye tamasha hili la Utamaduni wa Msukuma. Nawaomba muendelee kujitokeza kwa wingi ili kwa pamoja tusherehekee, tuhifadhi na kuenzi utamaduni wetu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Chifu Kidola wa Pili.
Kwa upande wake, Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Shinyanga, Innocent Mtafi, amesema tamasha hilo lina mchango mkubwa katika kulinda na kuendeleza utamaduni wa Mtanzania, huku likiwawezesha vijana kujifunza mila, desturi na historia ya jamii zao.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa utamaduni kuhakikisha sekta hiyo inapewa kipaumbele, kwa kuwa ni sehemu muhimu ya utambulisho wa Taifa na urithi unaopaswa kulindwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Naye mdau wa utamaduni kutoka Nairobi nchini Kenya, Dominic Mkami, wa kabila la Wakamba, amesema amesafiri hadi Shinyanga kushiriki tamasha hilo kwa lengo la kumuunga mkono mwandaaji wake, Peter Frank Lugumi maarufu Mr. Black, kutokana na juhudi zake za kuhifadhi, kuendeleza na kuitangaza tamaduni ya Wasukuma.
Mkami amesema tamasha hilo limekuwa daraja muhimu la kuunganisha jamii mbalimbali za Afrika Mashariki kupitia utamaduni, huku likitoa nafasi ya kubadilishana uzoefu, kuimarisha mahusiano ya kijamii na kukuza fursa za kiuchumi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Shinyanga Sukuma Festival & Business Expo, Peter Frank Lugumi (Mr. Black), amewataka wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki tamasha hilo linaloendelea hadi Julai 26, 2026.
Amesema mbali na burudani za ngoma za asili, wananchi na wageni watapata fursa ya kujifunza utamaduni wa Wasukuma, kutembelea mabanda ya biashara, kuona bidhaa mbalimbali pamoja na kushiriki shughuli tofauti zinazolenga kuonyesha utajiri wa utamaduni wa jamii hiyo.
Shinyanga Sukuma Festival & Business Expo Season 5 inaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha utamaduni, biashara na jamii, huku ikiweka mkazo katika kuhifadhi historia na urithi wa Wasukuma kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
TAZAMA VIDEO👇👇
















































































































Social Plugin