Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKAKATI WA WATALII MILIONI 8: TTB YAAGIZWA KUIBEBA SEKTA BINAFSI



Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, ametoa agizo zito kwa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) akitaka taasisi hiyo kuzingatia ubunifu, uwajibikaji, na uzalendo, huku ikihakikisha inashirikisha kikamilifu sekta binafsi katika kila hatua ya utekelezaji wa majukumu yake.

Akizungumza katika kikao cha tathmini na kuboresha utendaji kazi jijini Dar es Salaam, Dkt. Kijaji alisisitiza kuwa sekta binafsi inapaswa kuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya TTB, hasa katika kuandaa jumbe zinazopelekwa kwenye masoko ya kimataifa, ili nchi iweze kufikia na kuvuka lengo la kuwavutia watalii milioni nane na zaidi ifikapo mwaka 2030.

Ili kuongeza ushindani wa Tanzania duniani, Waziri Kijaji aliitaka bodi hiyo kuweka malengo yanayopimika na kufanya tafiti za kina zitakazofuatilia mwenendo wa masoko ya kimataifa. 

Alibainisha kuwa kwa sasa TTB ndiyo yenye dhamana kuu ya kuiuza nchi huko nje, hivyo inapaswa kuzishauri taasisi nyingine za kiserikali kama vile Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuhusu mahitaji halisi ya soko ili kuboresha huduma na bidhaa za utalii nchini. 

Vilevile, alihimiza utekelezaji wa mikakati ya pamoja kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akitaka taasisi zote kupanga mipango yao kwa ushirikiano ili kufikia malengo ya nchi kwa wakati.

Kuelekea matukio makubwa ya kimataifa yanayotarajiwa kufanyika nchini ikiwemo michuano ya AFCON na Mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Kijaji ameiagiza TTB kujipanga mapema na kikamilifu ili kutumia fursa hizo adhimu kuitangaza Tanzania na vivutio vyake duniani kote. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTB, Balozi Dkt. Ramadhani Kitwana Dau, alihakikisha kuwa bodi yake imeshaweka mikakati madhubuti ya kufikia malengo hayo ya serikali na kuvuka yale yaliyowekwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. 

Kikao hicho cha kimkakati kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbas, Mkurugenzi Mkuu wa TTB Ephraim Mafuru, pamoja na viongozi wengine waandamizi wa wizara na wajumbe wa bodi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com