Meneja mawasiliano na uhusiano wa Tume ya madini Greyson Mwase alievaa kifaa cha kisasa cha maabara cha X-Ray Fluorescence (XRF)kinachowezesha uchambuzi wa madini kwa haraka na kwa usahihi akiwa katika banda la Wizara ya madini katika maonesho ya 50 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam (DITF)akionesha namna kifaa hicho kilivyo na uwezo wa kufanya kazi kwa haraka 
Baadhi ya wanafunzi waliotembelea banda la Wizara ya madini wakipima madini kwa kutumia kifaa cha kisasa cha maabara cha X-Ray Fluorescence (XRF) katika maonesho ya 50 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam (DITF)Na Mwandishi wetu Malunde 1-Blog Dar es Salaam
Tume ya madini imewaalika wawekezaji, wachimbaji wa madini, wadau wa sekta ya madini, wanafunzi na wananchi kutembelea banda la Wizara ya madini katika maonesho ya 50 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) ili kujionea fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya madini nchini.
Kupitia banda hilo lililopo katika viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere, Tume imeonesha utajiri wa rasilimali za madini za Tanzania huku ikitoa elimu kuhusu fursa za uwekezaji, taratibu za upatikanaji wa leseni za madini, huduma za udhibiti wa shughuli za madini pamoja na teknolojia za kisasa za uchunguzi na upimaji wa madini.
Akizungumza katika mahojiano maalum, meneja wa mawasiliano na uhusiano wa Tume ya madini, Greyson Mwase, amesema maonesho hayo ni jukwaa muhimu linalowawezesha wadau na wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu sekta ya madini na huduma mbalimbali zinazotolewa na Tume.
"Tunawakaribisha wadau wote pamoja na wananchi kutembelea banda letu ili kujifunza kuhusu utajiri wa rasilimali za madini zilizopo nchini, fursa za uwekezaji na huduma mbalimbali zinazotolewa na Tume ya madini.
Wataalamu wetu wapo tayari kutoa maelekezo kuhusu upatikanaji wa leseni za madini, uzingatiaji wa sheria na kanuni, pamoja na huduma za uchunguzi na upimaji wa madini," amesema Mwase.
Amesema Tume inaendelea kutekeleza dhamira ya Serikali ya kuongeza uelewa wa umma kuhusu sekta ya madini ili Watanzania na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wanufaike na fursa zinazotokana na maboresho yanayoendelea kufanyika katika sekta hiyo.
Mbali na kutoa elimu kuhusu uwekezaji, Tume pia imeonesha huduma za maabara ya kisasa ya X-Ray Fluorescence (XRF) inayowezesha uchambuzi wa madini kwa haraka na kwa usahihi, hatua inayorahisisha shughuli za wachimbaji na wawekezaji.
Aidha, wananchi wanaotembelea banda hilo wanapatiwa elimu kuhusu uchimbaji unaozingatia utunzaji wa mazingira, afya na usalama mahali pa kazi pamoja na juhudi za Serikali za kuwawezesha wachimbaji wadogo kupitia urasimishaji wa shughuli zao, mafunzo na huduma za kitaalamu.
Mwase amesema maonesho hayo yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, jamii za wachimbaji na wawekezaji, huku yakiitangaza Tanzania kama kitovu cha uwekezaji katika sekta ya madini barani Afrika.
Ameongeza kuwa Tume ya madini itaendelea kutoa huduma na elimu kwa wadau wote watakaotembelea banda la Wizara ya madini katika kipindi chote cha maonesho hayo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kujenga sekta ya madini iliyo shindani, endelevu na yenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.



Social Plugin