Baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamewataka Watanzania kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi, wakieleza kuwa ndio msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hasa katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na wito unaosambazwa kupitia mitandao ya kijamii wa kufanya maandamano, huku Serikali ikisisitiza kuwa maandamano hayo hayataruhusiwa.
Akizungumza na Mwandishi wetu wa habari leo Jumatatu Julai 06, 2026 Mkazi wa Dar es Salaam, Bw. Fidelis Mrina, amesema vurugu zinazoambatana na maandamano huathiri moja kwa moja shughuli za biashara, kwani wafanyabiashara hulazimika kufunga biashara zao na kukimbia kwa hofu ya usalama, jambo linalosababisha hasara na kuhatarisha mitaji yao.
"Nina biashara, inapotokea vurugu nalazimika kukimbia, siwezi kufanya biashara na biashara yangu inakuwa hatarini kwa sababu vurugu haziwezi kuniacha salama." amesema Mrina.
Kwa upande wake, Bi. Janeth Yohana amesema amani ndiyo inayowawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa, akibainisha kuwa wanawake na watoto huwa katika hatari kubwa zaidi pindi machafuko yanapotokea. Amesema pia kuwa mafundisho ya dini yanasisitiza umuhimu wa kulinda amani na kuishi kwa upendo.
Naye Bw. Hassan Kondo amesema hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana bila kuwepo kwa amani, akieleza kuwa mshikamano na kupendana miongoni mwa wananchi ndiyo njia bora ya kuendelea kuijenga Tanzania yenye utulivu, akisisitiza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kulinda amani ili kuhakikisha shughuli za uzalishaji, biashara na utoaji wa huduma zinaendelea bila vikwazo.
Kauli za wananchi hao zinakuja wakati Serikali ikiendelea kusisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria na kudumisha utulivu wa nchi, huku ikionya dhidi ya ushiriki katika maandamano yanayohamasishwa kupitia mitandao ya kijamii ambayo yamepigwa marufuku, ikieleza kuwa amani ni nguzo muhimu ya maendeleo na ustawi wa Taifa.


Social Plugin