Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBUNGE ASHA MOTO AIPONGEZA SERIKALI-UWEKEZAJI GESI ASILIA


Mtwara Juni 11, 2026

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mtwara, Mhe. Asha Moto, amepongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya gesi asilia kupitia TPDC, alisema uwekezaji huo unachangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi.

Mhe. Moto alisema hayo alipotembelea Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia cha Madimba akiwa ameambatana na ujumbe wa zaidi ya viongozi 100 ambao ni waheshimiwa madiwani wa Viti Maalumu na wajumbe wa kamati ya Utekelezaji UWT kutoka Halmashauri za Mtwara Mjini, Mtwara vijijini, Newala, Nanyumbu, Tandahimba na Masasi kwa lengo la kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika sekta hiyo.

"Tumeshuhudia uwekezaji mkubwa uliofanywa katika Kiwanda cha Madimba unaodhihirisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha rasilimali za gesi asilia zinachangia uchumi wa taifa na kuboresha maisha ya wananchi. Nawapongeza TPDC kwa kazi kubwa wanayoifanya na nitoe wito kwa Watanzania kuendelea kulinda miundombinu ya gesi asilia," alisema Mhe. Moto.

Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalumu wa Halmashauri ya Newala, Mhe. Siwanina Mohamed Jaziri, alisema ziara hiyo imewaongezea uelewa kuhusu sekta ya gesi asilia na kuwawezesha kuwa mabalozi wa kutoa elimu sahihi kwa wananchi kuhusu manufaa ya rasilimali hiyo.

Katika hatua nyingine, Msimamizi wa Kiwanda cha Kuchakata gesi asilia cha Madimba, Mhandisi Kassimu Mkombwa, alisema kiwanda hicho huchakata na kusafirisha gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha umeme, viwandani, kwenye magari na matumizi mengine ya kiuchumi, huku kikizingatia viwango vya kimataifa vya usalama na utunzaji wa mazingira.

Akihitimisha ziara hiyo, Mhe. Asha Moto alisema uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali katika sekta ya gesi asilia unaonesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha rasilimali hiyo inachochea ukuaji wa uchumi, maendeleo ya viwanda na ustawi wa Watanzania.

Aidha, aliipongeza TPDC kwa kusimamia kwa ufanisi Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia cha Madimba kwa kutumia wataalamu wake wa ndani, jambo ambalo linaonesha uwezo wa Watanzania katika kusimamia miundombinu ya kimkakati ya sekta ya mafuta na gesi kwa weledi, ufanisi na kuzingatia viwango vya kimataifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com