
Serikali imesisitiza kuwa maendeleo ya kweli na ya kudumu ya Taifa yanategemea kwa kiasi kikubwa ujenzi wa wananchi wenye maadili, uzalendo, uwajibikaji na mshikamano thabiti.
Akizungumza jijini Dar es Salaam alipokutana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba alibainisha kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika kuboresha tabia za wananchi na kuimarisha utendaji kazi wa taasisi za umma ili kulinda haki za wananchi na kuimarisha amani nchini.
Aidha, serikali imeahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na Taasisi ya Mwalimu Nyerere katika kukuza umoja wa kitaifa na kuunga mkono ujenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere.
Kwa upande wake, Joseph Butiku alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake thabiti na kumpongeza Waziri Mkuu kwa jinsi anavyomsaidia katika kusimamia shughuli za serikali na kutatua changamoto za wananchi kupitia ziara zake mikoani.
Butiku alitumia fursa hiyo kukemea tabia ya baadhi ya watu kuwavunjia heshima viongozi, wazee, na viongozi wa dini, akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kukosoana kwa hoja na kwa kufuata sheria huku wakilinda amani na mshikamano wa Taifa.
Vilevile, aliishukuru serikali kwa ushirikiano wake unaoendelea na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, pamoja na kuipongeza kwa kuchukua hatua za kuimarisha misingi ya demokrasia, haki za watu, utawala wa sheria, na kutoa kipaumbele suala la Katiba Mpya kupitia Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030.
Social Plugin