MADEREVA wa bodaboda mkoani Dar es Salaam wameanza kunufaika na kampeni ya usalama barabarani itakayowapatia elimu pamoja na vifaa kinga, ikiwemo reflecta na miwani, kwa lengo la kupunguza madhara yanayotokana na ajali za barabarani.
Kampeni hiyo inayoitwa “Kuwa Makini Okoa Maisha” imeanzishwa na Chama cha Watalaam wa Afya na Usalama Mahala Pa kazi Tanzania(TOHASA) kwa kushirikiana na OSHA, WCF, SAFETY AND SECURITY, JAFFERJEE na TMHS GROUP ambapo kampeni imeanza rasmi leo Julai 25, 2026, katika eneo la Tangi Bovu-Kawe, wilayani Kinondoni, mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza na madereva wa bodaboda katika eneo hilo, Rais wa TOHASA, Caroline Baraza, amesema wameamua kuanzisha kampeni hiyo ili kuongeza uelewa wa madereva kuhusu usalama barabarani na umuhimu wa kuheshimu sheria na taratibu wakati wa kutumia barabara.
Amesema ajali nyingi zinazotokea barabarani zinaweza kupunguzwa iwapo madereva watapatiwa elimu ya kutosha kuhusu namna ya kutumia barabara na hatua wanazopaswa kuchukua ili kujilinda wao pamoja na abiria.
“Lengo ni kuwapatia elimu maofisa usafirishaji ili wawe makini na kuheshimu sheria kwa sababu tunaangalia ajali nyingi zinazotokea na takwimu zinaonesha watu wengi wanakosa elimu na kutokujua wafanye nini wakati gani,” amesema Baraza.
Amesema lengo kuu la kampeni hiyo ni kuokoa maisha, ndiyo maana TOHASA imeamua kutumia kaulimbiu ya “Kuwa Makini Okoa Maisha” katika kampeni hiyo.
Baraza ametoa wito kwa madereva wa bodaboda kuhakikisha wanazingatia sheria za barabarani, akisisitiza kuwa sheria hizo zinalenga kulinda watumiaji wote wa barabara bila kujali aina ya chombo wanachotumia.
Amesema madereva wanapaswa pia kuwa mabalozi wa usalama kwa kuwaelimisha wenzao pale wanapoona wakifanya vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha.
“Wito wa TOHASA kwa maofisa usafirishaji wafuate sheria za barabarani kwani hazina mtu huyu na huyu, bali ziko kwa ajili yetu sote tunaotumia barabara. Pia kuwa makini pale inapobidi, unapoona mwenzako anavunja sheria wewe kuwa makini na mfundishe au kumuelekeza,” amesema.
Amesema TOHASA inajumuisha wataalamu kutoka hospitali na taasisi mbalimbali zinazotoa huduma kwa watu wanaopata dharura barabarani, hivyo wanaona umuhimu wa kuwekeza zaidi katika elimu ya kuzuia ajali kabla hazijatokea.
Kwa upande wake, Mkuu wa Usalama Barabarani Wilaya ya Polisi Kawe/Mbweni, Mkoa wa Kinondoni, Adrian Kamara, amesema Jeshi la Polisi limeendelea kushirikiana na TOHASA katika kutoa elimu kwa madereva wa pikipiki kuhusu matumizi salama ya barabara.
Kamara amesema kupitia kampeni hiyo wamewakumbusha madereva kuzingatia usalama wao na abiria, kutumia barabara kwa usahihi pamoja na kuheshimu sheria za usalama barabarani.
“Tumeshirikiana na TOHASA ambao wanahusika na usalama mahala pa kazi kuwakumbusha madereva pikipiki kuzingatia usalama na abiria pamoja na utumiaji sahihi wa barabara, watii sheria za usalama barabarani kwa maana ya kuheshimu vivuko, kutokuendesha pembeni ya barabara,” amesema.
Amesema madereva wa bodaboda ni watumiaji rasmi wa barabara na wanatambulika kisheria, hivyo wanapaswa kutumia barabara kwa utaratibu unaotakiwa kama ilivyo kwa watumiaji wengine.
“Tumewafahamisha wao ni watumiaji rasmi na wanatambulika kisheria, hivyo waendeshe pikipiki zao katikati ambako ni sehemu sahihi, kama ni kushoto au kulia kufuata utaratibu kama magari yanavyotembea,” amesema.
Kamara pia amesisitiza umuhimu wa madereva hao kuvaa viakisi mwanga (reflecta), hasa wakati wa usiku au katika maeneo yenye mwonekano hafifu, ili waweze kuonekana kwa urahisi na madereva wengine.
Amesema pia wamewakumbusha madereva kuvaa kofia ngumu wakati wote wanapoendesha pikipiki, bila kujali umri, ili kupunguza madhara endapo ajali itatokea.
Katika kampeni hiyo, TOHASA imewapatia madereva reflecta pamoja na miwani kwa ajili ya kujikinga na vumbi, ikiwa ni sehemu ya hatua za kuwawezesha kufanya kazi katika mazingira salama zaidi.
Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa TOHASA, Gerald Mrema, amesema taasisi hiyo imeamua kuendesha kampeni hiyo kutokana na ongezeko la vifo, majeruhi na ulemavu wa kudumu unaosababishwa na ajali za barabarani.
Mrema amesema TOHASA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na taasisi mbalimbali zinazotoa vifaa kinga vya usalama mahali pa kazi, imeona umuhimu wa kuwafikia madereva wa bodaboda moja kwa moja na kuwapatia elimu pamoja na vifaa vitakavyowasaidia kujilinda.
“Taasisi yetu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na taasisi mbalimbali ambazo zinatoa vifaa kinga vya usalama mahala pa kazi tumetoa elimu kwa bodaboda tukiwa na kusudi kubwa baada ya elimu hii watahakikisha wanaendesha vyombo vya moto kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi, kwa kufuata alama za barabarani na kutopakia abiria zaidi ya mmoja,” amesema Mrema.
Aidha, Mrema amesisitiza umuhimu wa madereva kuhakikisha wanatumia vifaa kinga wanapokuwa kazini, akisema reflecta ni muhimu kwa sababu husaidia madereva kuonekana kwa mbali, hasa nyakati za usiku.
Amesema pia madereva wanapaswa kuvaa viatu kinga ambavyo vinaweza kusaidia kulinda miguu yao endapo ajali itatokea.
Mrema amewataka madereva kuwa na utaratibu wa kukagua pikipiki zao mara kwa mara, hususan asubuhi kabla ya kuanza kazi, ili kuhakikisha vyombo hivyo viko katika hali nzuri na salama kwa matumizi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tangi Bovu, Athuman Kitunguu, amesema wamepokea kwa furaha elimu ya usalama barabarani pamoja na vifaa kinga walivyopatiwa na TOHASA.
Kitunguu amesema eneo hilo limekuwa likikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ajali za barabarani, hivyo elimu hiyo itawasaidia madereva kuongeza umakini na kuzingatia sheria.
“Kwasasa tunashukuru Jeshi la Polisi limekuwa linatupa ushirikiano mzuri na elimu ambazo tunapatiwa zinatuongezea uelewa kuhusu kufuata sheria za usalama barabarani,” amesema.
Amesema elimu ya usalama barabarani inapaswa kuendelea kutolewa mara kwa mara kwa madereva ili kuongeza uelewa na kuhamasisha matumizi ya vifaa kinga, hatua ambayo itasaidia kupunguza ajali na madhara yake.





















Social Plugin