
Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Juni 4, 2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la papo kwa papo la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Asha Salum Moto, ambaye alitaka kujua namna Serikali ilivyojipanga kukabiliana na ugonjwa wa Ebola unaoripotiwa katika baadhi ya nchi jirani.
"Mpaka sasa tuko salama, nchi yetu iko salama. Ni jambo la kumshukuru Mungu. Hata hivyo, kwa kuwa Tanzania si kisiwa, tunaendelea kuchukua hatua zote za tahadhari ili kuhakikisha usalama wa wananchi wetu unaendelea kuwepo," amesema Dkt. Mwigulu.
Amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko, kuimarisha ufuatiliaji mipakani pamoja na kuhimiza utoaji wa taarifa mapema pale dalili za magonjwa hayo zinapojitokeza.
"Tuendelee kuzingatia ushauri wa wataalam wa afya na tusifiche dalili wala taarifa zinazoweza kusaidia kuzuia kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko," amesema.
Katika swali jingine, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya reli na miundombinu mingine ya usafiri ili kukabiliana na changamoto zinazotokana na ukuaji wa miji na kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi.
Kauli hiyo ameitoa alipokuwa akijibu swali la papo kwa papo la Mbunge wa Kigamboni, Mhe. Haran Sanga, ambaye alitaka kujua mpango wa Serikali wa kuimarisha miundombinu ya reli katika majiji yanayokuwa kwa kasi nchini.
"Serikali tayari imeanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara za mzunguko katika miji mikubwa na kukamilisha miradi ya reli ya kimkakati. Kadri hali ya kifedha itakavyoruhusu, tutaendelea kuwekeza pia katika reli za ndani ya majiji yetu," amesema.
Aidha, akijibu swali la Mbunge wa Mvomero, Mhe. Sarah Msafiri, ambaye alitaka kujua mpango wa Serikali wa kuwekeza kikamilifu katika kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji, kuchochea ukuaji wa uchumi na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Waziri Mkuu amesema Serikali imeongeza uwekezaji katika sekta hiyo na kuendelea kufufua miradi mbalimbali ya umwagiliaji nchini.
"Kwa nchi ambayo zaidi ya asilimia 65 ya wananchi wake wanategemea kilimo, umwagiliaji ni ufumbuzi wa changamoto nyingi ikiwemo kuongeza uzalishaji, kipato na usalama wa chakula," amesema.
Amesema Serikali imefufua mamia ya miradi ya umwagiliaji, inaendeleza mabonde ya maji na inaendelea kutekeleza mpango wa muda mrefu wa kusambaza maji kutoka katika vyanzo vya kudumu kwa matumizi ya majumbani, umwagiliaji na shughuli za ufugaji.
Kadhalika, akijibu swali la Mbunge wa Mafinga Mjini, Mhe. Dickson Nathan Lutevele, ambaye alitaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha wakulima wa mazao ya biashara wanalipwa kwa wakati ili waendelee kuimarisha uzalishaji, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuboresha masoko ya mazao, kuongeza uwezo wa uchakataji ndani ya nchi na kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta hiyo.
"Tumekuwa tukifanya vikao na wadau wa mazao mbalimbali ikiwemo chai, tumbaku, pamba na korosho ili kuhakikisha wakulima wanapata masoko ya uhakika na malipo yanayostahili kwa wakati," amesema.
Amesema Serikali itaendelea kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya uchakataji wa mazao ya kilimo ili kuongeza thamani ya mazao, kupanua masoko na kuongeza mapato kwa wakulima.






Social Plugin