Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHEIKH PEMBE ASISITIZA KUHUSU UMUHIMU WA AMANI, ATAKA WAISLAMU KUILINDA NCHI YAO



Imamu Mkuu Masjid Mtambani Sheikh Shabani Pembe amewataka Waislamu na Watanzania wote kwa ujumla kuendelea kudumisha na kuilinda amani ya Tanzania, akisisitiza kuwa ikiwa serikali ingeruhusu kufanyika kwa kile kilichokuwa kimepangwa, kuratibiwa na kuhamasisha Oktoba 29, 2025 basi Tanzania isingeweza kukalika tena kutokana na uvunjifu wa amani ambao ungetokea wakati ule wa Uchaguzi.

Sheikh Shabani Pembe amebainisha hayo wakati akitoa hotuba yake kwa waumini wa Dini ya Kiislamu Mkoani Dar Es Salaam na kuwataka Waislamu kuhukumu kile kilichotokea kwa uadilifu pamoja na kupima athari ambazo zingeweza kujitokeza ikiwa serikali ingewaaacha wale waliokuwa wamejitokeza barabarani kuendelea na matukio yao ya uvunjifu wa amani Nchini.

"Kituo chetu cha mwendokasi tumeshuhudia kikichomwa, Vituo vya Polisi vilichomwa, ATM pale Manyanya imechomwa na hata maduka ya watu yamechomwa na kuibiwa, hawa watu wangeachiwa wafanye wanavyotaka hii Nchi ingekuwa wapi? Ndugu zangu tunapohukumu tuhukumu kwa uadilifu, kwamba lengo lilikuwa waachiwe wafanya wanavyotaka? Au ilikuwa nini? Baadae wale wote waliowachochea wanaanza kuiona dola mbaya, Tunapohukumu mambo tuhukumu kwa uadilifu." Amesema Sheikh Pembe.

"Tunapohukumu mambo tuhukumu kwa uadilifu, amani ni tunu ndugu zangu, ikiondoka hii hata sisi hatuwezi kukusanyika. Ile Ijumaa ile kutoka Tegeta mpaka hapa nililipa Elfu sitini kwa bodaboda na nimefika hapa naambiwa Mufti ametangaza hakuna ibada hapa, sasa waislamu niwaombe kuipenda Nchi yako ni katika Imani. Wale wote waliokuwa wanahamasisha yale ya Oktoba 29 hakuna hata mtoto wao aliyeguswa na kiwembe, tafsiri yake ni kuwa wao na familia zao zilibaki salama, kinyume chake familia za maskini na fukara ndio waliotolewa kafara." Ameongeza kusema.

Sheikh Pembe amewakosoa vikali pia wale wanaokosoa Tume zilizoundwa kuchukua matukio hayo ya wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisisisitiza kuwa Tanzania ni huru na Watanzania wanapaswa kuunga mkono busara na hekima za Viongozi wao katika kupata muafaka na suluhu ya kudumu dhidi ya kile kinachotajwa kama sababu ya matukio ya Oktoba 29, 2025.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com