Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CCM :TANZANIA INAHITAJI UJENZI WA HOJA ,SIYO MAANDAMANO NA VURUGU



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitaendelea kusimamia siasa za maendeleo na utatuzi wa changamoto za wananchi, kikisisitiza kuwa dira yake ni kuhudumia wananchi badala ya kufanya siasa za matukio.

Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari Leo June 13,2026 Jijini Dodoma, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, amesema CCM imejikita katika kutekeleza majukumu yake kwa kushughulikia changamoto zinazowakabili Watanzania na kusukuma mbele agenda ya maendeleo.

Amesema katika ziara mbalimbali ambazo chama kimefanya nchini, viongozi hukutana na wananchi kupitia mikutano ya hadhara na kusikiliza kero zao ili kutafuta majawabu ya changamoto zinazowagusa moja kwa moja.

“CCM si chama cha matukio,tunafanya kazi ya kutatua changamoto za wananchi na kuhakikisha maendeleo yanafika katika kila sekta,tunampongeza Mwenyekiti wetu kwa uongozi wake makini ambao umewezesha kupatikana kwa mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali za maendeleo,” amesema.

Kihongosi amesema chama kinafahamu kuwa wananchi wanahitaji huduma bora za afya, maji safi na salama, elimu, miundombinu na huduma nyingine za msingi, hivyo Serikali ya CCM imeendelea kuelekeza nguvu katika maeneo hayo.

Akizungumzia hali ya kisiasa nchini, amesema CCM imepokea taarifa kuhusu madai ya kuwepo kwa mikutano ya siri inayodaiwa kufanywa na baadhi ya viongozi wa upinzani kwa lengo la kuhamasisha maandamano na vitendo vinavyoweza kuvuruga amani.

Kutokana na hali hiyo, ametoa wito kwa Watanzania kutoruhusu makundi yoyote ya wanaharakati au vyama vya siasa kutumia ajenda za maandamano na vurugu ambazo zinaweza kuhatarisha utulivu uliopo nchini.

“Tunatoa rai kwa wazalendo wote na wapenda maendeleo kutoshabikia maandamano na vurugu kwa namna yoyote ile. Tanzania imejengwa katika misingi ya amani, mshikamano na utulivu, na tunapaswa kuilinda misingi hiyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema.

Aidha, amesema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia majukwaa mbalimbali kuchochea migawanyiko na vurugu, huku akisisitiza kuwa taifa halipaswi kuruhusu vitendo vinavyoweza kuhatarisha uhuru na mshikamano wa wananchi.

Kihongosi ameeleza kuwa mara nyingi madhara ya maandamano hubebwa na wananchi wa kawaida, hususan wafanyabiashara wadogo, wafanyakazi na vijana, wakati familia za viongozi wa kisiasa mara nyingi haziguswi moja kwa moja na athari hizo.

“Tunahitaji Tanzania inayojenga hoja kupitia majadiliano ya kidemokrasia, siyo kupitia vurugu au uharibifu wa mali na maisha ya wananchi,” amesema.

Pia ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kudumisha umoja wa kitaifa na kutoruhusu kugawanywa kwa misingi ya dini, kabila, eneo au itikadi za kisiasa.

Amesema nguvu ya taifa ipo katika mshikamano wake, na kwamba tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa chanzo cha chuki au migawanyiko inayoweza kuhatarisha amani na maendeleo ya nchi.

Katika hatua nyingine, ameviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuwa macho na kutekeleza wajibu wao wa kulinda amani na usalama wa raia na mali zao, huku akiwahimiza wananchi kushirikiana navyo kwa kutoa taarifa pale wanapoona viashiria vya uvunjifu wa amani.

Akizungumzia bajeti ya Serikali iliyosomwa hivi karibuni bungeni, Kihongosi amesema imeonyesha hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi na kuimarika kwa uwezo wa nchi kujitegemea kiuchumi.

Amepongeza Serikali pamoja na Bunge kwa kazi kubwa ya kuandaa na kupitisha bajeti hiyo, akisema itaendelea kuchochea maendeleo ya taifa na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com