Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Katika hatua inayoashiria mwanzo wa enzi mpya ya matumizi ya nishati safi nchini, Serikali imezindua rasmi vituo vya kwanza vya kuchajia magari yanayotumia umeme sambamba na mpango wa kuwawezesha wananchi kupata majiko ya umeme kwa mkopo kupitia mfumo wa ununuzi wa LUKU.
Mpango huo unalenga kuharakisha matumizi ya nishati ya umeme majumbani na katika sekta ya usafiri, huku ukipunguza utegemezi wa kuni na mkaa ambao kwa muda mrefu umechangia uharibifu wa mazingira na athari za kiafya.
Akizindua miradi hiyo jijini Dodoma, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, alisema Serikali imefikia hatua hiyo kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme nchini, jambo linalowezesha wananchi kutumia nishati hiyo kwa wigo mpana zaidi katika shughuli za kila siku.
Alieleza kuwa mfumo wa majiko ya umeme kwa mkopo utawaruhusu wananchi kuyapata bila kulazimika kutoa fedha nyingi kwa wakati mmoja, badala yake wakilipa kwa awamu kupitia huduma ya LUKU.
Kwa upande wa miundombinu ya usafiri wa kisasa, Waziri huyo alisema vituo vya kuchajia magari ya umeme vitaongeza imani kwa wawekezaji na watumiaji wa teknolojia hiyo, huku Serikali ikitangaza kuwa kwa siku 30 za mwanzo huduma za kuchaji zitatolewa bila malipo ili kuhamasisha matumizi yake.
Hatua hiyo inatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Serikali wa kujenga uchumi wa kijani unaotegemea nishati safi, kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kufungua fursa mpya za uwekezaji, ajira na ubunifu katika sekta ya teknolojia.
Kwa kuzinduliwa kwa programu hizi mbili muhimu, Tanzania inaweka msingi wa safari mpya ya maendeleo ambapo matumizi ya umeme yanatarajiwa kuwa kichocheo kikuu cha mageuzi ya kiuchumi, uhifadhi wa mazingira na ustawi wa wananchi.



Social Plugin