Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KPMG YAHAMASISHA VIJANA KUHIFADHI MAZINGIRA


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Kampuni ya KPMG Tanzania imeamua kuendelea kudhamini shughuli mbalimbali zinazohamasisha utunzaji wa mazingira kwa vijana na wanafunzi ikiwa ni sehemu ya mchango wao katika kulinda mazingira nchini.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani , Frank Mboya amesema KPMG imekuwa ikishiriki katika utoaji wa elimu pamoja na udhamini wa mashindano mbalimbali mashuleni yanayolenga kuwajengea vijana uelewa kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira.

Amesema kampuni hiyo ambayo ni moja kati ya makampuni makubwa manne duniani yanayojihusisha na ukaguzi wa mahesabu, uhasibu na ushauri wa kitaalamu, imeona umuhimu wa kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha kizazi kijacho kinakuwa na uelewa mkubwa kuhusu uhifadhi wa mazingira.

Mboya amesema mbali na kutoa elimu, KPMG pia imekuwa ikitoa zawadi kwa washindi wa mashindano mbalimbali kama njia ya kuwahamasisha wanafunzi kushiriki kwenye shughuli za mazingira.

Aidha, amesema dunia kwa sasa imeanza kuelekeza nguvu kubwa kwenye masuala ya mazingira ambapo baadhi ya kampuni na taasisi zimeanza kutakiwa kujumuisha taarifa za mazingira katika ripoti zao za kifedha.

Amesema lengo kubwa ni kuhakikisha dunia inaendelea kuwa salama na ya kijani kwa vizazi vijavyo kupitia ushirikiano wa sekta binafsi, serikali pamoja na jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com