Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ZAIDI YA VIJANA 200 KUTOKA MATAIFA MBALIMBALI WAKUTANA ARUSHA KUPINGA DAWA ZA KULEVYA


Na Bora Mustafa, Arusha

Zaidi ya vijana 200 kutoka mataifa mbalimbali duniani wamekutana jijini Arusha katika Kongamano la Kwanza la Vijana Barani Afrika kuhusu Mapambano dhidi ya Matumizi ya Dawa za Kulevya, wakilenga kujadili mbinu za kukabiliana na tatizo hilo na kuimarisha ushiriki wa vijana katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

Washiriki wa kongamano hilo wanatoka katika nchi mbalimbali ikiwemo Afrika Kusini, Malawi, Kenya, Uganda, Rwanda na Uturuki, ambapo wanapata fursa ya kubadilishana uzoefu, kujifunza kutoka kwa wataalamu na kujenga mtandao wa ushirikiano katika mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya.

Akizungumza wakati wa kongamano hilo, Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Taasisi ya Care for All, Hawa Omani, alisema jukwaa hilo limeandaliwa kwa lengo la kuwajengea vijana uwezo wa kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii zao na kuongeza uelewa kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya.

Alisema kongamano hilo linafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kimataifa miongoni mwa vijana wa Afrika na mataifa mengine katika kutafuta suluhisho la kudumu dhidi ya changamoto ya dawa za kulevya.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, alisema elimu ni silaha muhimu katika mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya, hususan kwa vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa.

Alisema ushirikiano wa familia, taasisi za elimu, viongozi wa jamii na wananchi kwa ujumla ni muhimu katika kuhakikisha kizazi kijacho kinakuwa salama dhidi ya athari za dawa za kulevya.

Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na mamlaka husika kwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vinavyohusiana na matumizi na biashara ya dawa za kulevya ili kusaidia kulinda afya ya jamii na mustakabali wa taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com