Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HATUNA UPANDE, TUNAFANYA KAZI NA KILA MTU- RAIS SAMIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa Tanzania haitachagua upande katika siasa wala mivutano ya kiitikadi inayovuta mataifa makubwa duniani bali itaendelea kusimamia misingi ya kutofungamana na upande wowote ikichukua fursa za kiuchumi kutoka vitalu vyote kwa maslahi ya taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari alioambatana nao katika ziara yake ya kiserikali jijini Moscow nchini Urusi, Rais Samia amebainisha kuwa nchi itashirikiana na Marekani, Ulaya, China, Urusi na Asia kwa usawa.

"Tumchukue Ulaya, Ulaya ni mshirika wetu kwenye biashara akichukua mazao mengi kutoka kwetu na sisi tunaagiza bidhaa kwao, twende Marekani, naye ni mshirika wetu mkubwa sana na ndio Nchi inayoongoza kwa kuleta watalii Nchini lakini pia tuna Makampuni zaidi ya 420 za kwenye sekta zote, Marekani pia ni mshirika mkubwa kwenye uwekezaji wa Tanzania. 

Tunapokuja Urusi nao wenyewe kutokana na vikwazo wanavyowekewa na mabadiliko ya siasa za dunia na sisi pia kuwa na mabadiliko kadhaa ya kisiasa yalituweka kando na Urusi lakini kwasasa hatuchagui wa kufanya nae kazi, tunakusanya wote na tunafanya nao kazi." Amesema Rais Samia.

Mkuu huyo wa nchi amefafanuzi kuwa diplomasia ya kisasa ya kiuchumi inaitaka serikali kufungua milango kwa kila mwekezaji, huku akichambua kwa kina miradi ya kimkakati inayounganisha Tanzania na mataifa ya Magharibi pamoja na sababu zilizosababisha ukimya wa kiushirikiano na Urusi tangu miaka ya 1980.

Rais Samia ameweka wazi kuwa msimamo wa kufungua milango kwa Urusi haumaanishi nchi inatupa washirika wake wa kihistoria wa Magharibi, ambao uwekezaji wao ni mkubwa nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com