Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

FISI: JE, TAMADUNI ZETU ZIMEKUWA KIFUNGO CHAKE?






Na Beatus Maganja

Tunapomfunga kwa minyororo, tunahifadhi utamaduni au tunamnyang'anya uhuru wake?

Umewahi kujiuliza fisi anapenda maisha gani? Je, anatamani kuishi akiwa amefungwa kwa kamba na minyororo ndani ya nyumba za binadamu? Je, anafurahia kutembelezwa mitaani kwa ajili ya burudani? Au kama angepewa nafasi ya kuchagua, angekimbilia hifadhini ambako ndiko nyumbani kwake ?
Maswali haya yameibuka tena baada ya hivi karibuni kurushwa kwa makala katika moja ya vituo vya televisheni nchini ikionesha baadhi ya maeneo ya Kanda ya Ziwa ambako bado kuna mila na desturi za kufuga fisi kama sehemu ya urithi wa kitamaduni unaopitishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.

Ni kweli, tamaduni ni sehemu muhimu ya utambulisho wetu. Zinabeba historia, maarifa na simulizi za mababu zetu. Lakini swali kubwa la kujiuliza ni hili...Je, kila tamaduni ya kale inapaswa kuendelea bila kuangalia athari zake kwa viumbe wengine?

Fisi ni mnyama wa porini. Ameumbwa kukimbia kilomita nyingi kutafuta chakula, kuwasiliana na kundi lake kupitia sauti za kipekee na kuzunguka katika maeneo makubwa ya asili. Anapofungwa kwa minyororo na kamba au kuwekwa katika mazingira yasiyo ya asili yake, sehemu kubwa ya uhuru wake hupotea.

Pengine hatuoni maumivu yake kwa sababu hawezi kuzungumza lugha yetu. Hatuwezi kusikia malalamiko yake wala kuona machozi yake. Lakini ukweli ni kwamba mnyama huyu, kama walivyo viumbe wengine, huhitaji nafasi, uhuru na mazingira yanayomruhusu kuishi maisha aliyoumbiwa.

Wataalamu wa uhifadhi wamekuwa wakisisitiza kuwa wanyamapori wana nafasi muhimu katika mifumo ya ikolojia. Fisi, ambaye mara nyingi huchukuliwa vibaya na baadhi ya watu, ni mmoja wa wasafishaji wakubwa wa mazingira ya porini. Hula mizoga na kusaidia kuzuia kuenea kwa magonjwa ambayo yangetokana na mabaki ya wanyama waliokufa.

Tunapomtoa porini na kumweka kifungoni kwa ajili ya desturi au burudani, si tu kwamba tunamnyima uhuru wake, bali pia tunapunguza mchango wake katika mazingira ya asili.

Hii haimaanishi kuwa tunapaswa kuzipuuza tamaduni zetu. La hasha. Badala yake, tunapaswa kutafuta namna ya kuzihifadhi kwa njia zinazokwenda sambamba na uelewa wa kisasa kuhusu ustawi wa wanyama na uhifadhi wa maliasili. Tunaweza kuenzi historia ya mila hizo kupitia simulizi, makumbusho, maonesho ya kitamaduni na elimu kwa vijana bila kuwafanya wanyamapori kuwa wafungwa wa tamaduni hizo.

Kadiri tunavyozidi kuelewa hisia na mahitaji ya viumbe wengine, ndivyo tunavyozidi kuwa walinzi bora wa uumbaji. Fisi, kama walivyo tembo, simba, pundamilia na wanyamapori wengine, hawakuumbwa kwa ajili ya minyororo. Waliumbwa kwa ajili ya uhuru.

Labda wakati umefika wa kujiuliza tena, Je, tunataka kurithisha vizazi vijavyo kumbukumbu za fisi waliofungwa, au tunataka kurithisha Tanzania yenye wanyamapori walio huru katika mazingira yao ya asili?

Jibu liko mikononi mwetu. 

📞 +255 676 475 541

#tawatanzania #tumerithishwa #tuwarithishe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com