Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BOT YAKUSANYA TANI 27.05 YA DHAHABU YENYE THAMANI YA TRILIONI 10



Na mwandishi wetu,Dar

Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 12 Juni 2026 amepongeza hatua kubwa iliyofikiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya kukusanya tani 27.05 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi trilioni 10 za Kitanzania.

Rais Samia ameyasema hayo leo Ijumaa Juni 13, 2026, aliposhiriki kama Mgeni Rasmi kwenye kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 tangu kuanzishwa kwa benki hiyo. Hafla hiyo kubwa imefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) uliopo jijini Dar es Salaam.

"Nipongeze Benki Kuu kwa mpango wa ununuzi wa dhahabu ya ndani. Hadi kufikia mwezi Mei mwaka huu, kama alivyosema mwenyewe Gavana, akiba yetu rasilimali yetu ya dhahabu tuliyoikusanya ni tani 27.5, yenye thamani ya shilingi trilioni 10 za Kitanzania. Hapa tulipofika, si haba." Amesema Rais Samia

Katika hotuba yake, Rais Samia amesisitiza kuwa ununuzi wa dhahabu ya ndani ni mkakati imara wa kuimarisha akiba ya fedha za kigeni nchini, akisema hatua hiyo inasaidia katika kulinda thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya mtikisiko wa kiuchumi duniani.

Rais amebainisha kuwa mkakati huo unalenga pia kujenga uchumi imara na unaojitegemea kwa faida ya kizazi cha sasa na cha baadaye, akitoa wito kwa Benki Kuu kuendelea kusimamia sekta ya fedha kwa umakini mkubwa ili kudhibiti mfumuko wa bei.

Amewataka kuendeleza ubunifu katika mifumo ya kidijitali ili kurahisisha huduma za kibenki kwa wananchi wote, hasa waishio vijijini akiweka wazi kuwa ukuaji wa sekta ya fedha unapaswa kwenda sambamba na maisha halisi ya Watanzania wa kawaida.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com