Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Serikali imekamata zaidi ya tani 1,017 za bangi katika kipindi cha mwaka 2025, huku ikieleza kuwa operesheni kali dhidi ya mitandao ya biashara ya dawa za kulevya zimeanza kuzaa matunda nchini.
Taarifa hiyo imetolewa LeoMei 29,2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, alipokuwa akiwasilisha taarifa ya hali ya dawa za kulevya nchini.
Prof. Kabudi amesema bangi imeendelea kuwa dawa ya kulevya inayoongoza kwa kukamatwa nchini ambapo jumla ya tani 1,017.26 zilikamatwa mwaka 2025, licha ya kiwango hicho kupungua kwa asilimia 55.97 ikilinganishwa na mwaka 2024.
Amesema kupungua huko kunatokana na operesheni za kuteketeza mashamba ya bangi, kuongezeka kwa doria katika maeneo hatarishi pamoja na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya dawa hizo.
“Tumeshuhudia mafanikio makubwa kutokana na ushirikiano wa vyombo vya usalama, serikali na wananchi katika kudhibiti biashara ya dawa za kulevya,” amesema Prof. Kabudi.
Mbali na bangi, serikali pia ilikamata tani 26.36 za mirungi mwaka 2025, kiwango kilichoonyesha ongezeko la asilimia 42.88 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Katika kundi la dawa za kulevya za viwandani, serikali ilikamata kilogramu 907.18 za methamphetamine, kilogramu 672.23 za heroin, kilogramu 4.89 za cocaine, gramu 178 za MDMA pamoja na gramu 7.82 za MDA.
Aidha, kwa mara ya kwanza nchini, serikali ilifanikiwa kukamata tani 29.52 za dawa mpya ya kulevya aina ya Kratom iliyokuwa imeingizwa nchini ikidaiwa kuwa mbolea.
Prof. Kabudi alisema uchunguzi wa kitaalamu ulibaini kuwa mzigo huo ulikuwa na dawa za kulevya zinazotokana na mmea ujulikanao kama Mitrogyna speciosa.
Katika hatua nyingine, alisema serikali pia ilikamata tani 31.76 na lita 183.5 za kemikali bashirifu pamoja na kilogramu 2.36 na mililita 160 za dawa tiba zenye asili ya kulevya zilizokuwa zikichepushwa kutoka matumizi yake halali.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mashauri 1,124 ya dawa za kulevya yalifunguliwa mahakamani mwaka 2025 huku mashauri 1,373 yakitolewa hukumu na serikali kushinda kesi 1,058.
Kadhalika, mali zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 3.3 zilizohusishwa na biashara ya dawa za kulevya zilitaifishwa.
Sambamba na operesheni hizo, watu 85,425 wenye uraibu wa dawa za kulevya walipata huduma za tiba na utengamao kupitia vitengo vya afya ya akili, kliniki za MAT na nyumba za upataji nafuu nchini.
Prof. Kabudi alisema licha ya mafanikio hayo, biashara na matumizi ya dawa za kulevya bado ni tishio kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa, hasa kwa vijana.
Alisema serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kitaifa na kimataifa katika kubadilishana taarifa za kiintelijensia, kufanya operesheni za pamoja pamoja na kuongeza uwezo wa taasisi zinazopambana na dawa za kulevya nchini.



Social Plugin