Waziri wa mambo ya ndani Nchini Tanzania Mhe. Patrobas Katambi ameonya kuwa Vyama vya siasa visipotumika vizuri na kutekeleza wajibu wake kisheria ni tishio kubwa kwa usalama wa Nchi, hasa pale viongozi wa Vyama hivyo watakapotumia ndimi na machapisho yao kuhamasisha vurugu badala ya mapatano.
Waziri Katambi ameeleza hayo leo Jumatatu Mei 25, 2026 Bungeni Mjini Dodoma wakati akihitimisha mjadala wa Bajeti ya Wizara ya mambo ya ndani kwa mwaka 2026/27, akisema Wizara yake itaendelea kusimamia na kukumbusha kuhusu taratibu, miongozo na sheria za Tanzania.
"Vyama vya siasa visipotumika vizuri Mhe. Spika ni tishio kubwa la usalama hasa pale Viongozi wa vyama hivi watakapotumia ndimi na kauli zao, maandiko na machapisho kuhamasisha vurugu na sio mapatano, pale watakapohamasisha wananchi kwenda kufanya mambo ambayo yanapelekea uvunjifu wa amani. Mhe Spika tutazidi kukumbushana na kusimamia taratibu kwasababu Wizara ya mambo ya ndani ni kitovu cha masuala yote ya amani, usalama na nidhamu ya Taifa kwenye utekelezaji wa sheria. Tutasimamia na kukumbusha wajibu wetu kila mmoja." Amesisitiza Waziri Katambi.
Amekosoa pia kuhusu baadhi ya wanasiasa kujificha kwenye mgongo wa haki za binadamu bila kutekeleza msingi wa wajibu wao, badala ya kulaumu na kukosoa serikali pale ambapo sheria zinapochukua mkondo wake, akisema wajibu wa Vyombo vya usalama ni kutafsiri sheria na kusimamia utii wa sheria Nchini

Social Plugin