Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Wizara ya mambo ya ndani Nchini Tanzania, kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo Nchini, imesisitiza kuwa kwa mwaka wa fedha 2026/27 imejizatiti vya kutosha kuhakikisha wanadhibiti na kuchukua hatua dhidi ya wizi na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii Nchini kwa kuhakikisha kuwa teknolojia haiwi sababu ya madhila na uvunjifu wa amani Nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Patrobas Katambi, leo Jumatatu Mei 25, 2026, Bungeni Mjini Dodoma wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara ya Mambo ya ndani kwa mwaka ujao wa fedha, akisema sheria ya huduma ya habari na ya kanuni ya adhabu inazuia kutweza utu wa mtu, kutoa taarifa za uongo au kudhalilisha mwananchi mwingine.
"Wapo watu wamejaribu kutweza utu na heshima za watu, wapo ambao wamewadhalilisha kwa kuwavumishia na kuwazushia mambo ya uongo na wapo pia ambao walipelekea kutoa taarifa za uongo, uzushi na uchochezi." Amesema Waziri Katambi.
Akitolea mfano wa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, Ameeleza kuhusu picha ilioonesha mfungwa mmoja akiwa amevalia hereni ilihali akiwa anatumikia kifungo chake gerezani, Waziri Katambi akisema picha ile imetengenezwa kwa akili unde kwa nia ya kuaminisha wengine kuwa mfungwa yule hakuwa mfungwa halali kama Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoelezwa.
Waziri Katambi akisisitiza kuhusu hatua ambazo wamezichukua, amebainisha kuwa tayari wizara yake imeketi vikao kadhaa na Mawaziri wa Wizara za Habari, utamaduni, sanaa na michezo pamoja na Waziri wa Teknolojia ili kwa pamoja kuchukua hatua kwa yeyote ambaye atatumia mtandao wa kijamii ama chombo cha habari kwaajili ya kueneza chuki, uongo na taarifa ambazo hazina ukweli.

Social Plugin