Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Katika shule nyingi za wanafunzi wenye mahitaji maalumu nchini, changamoto ya kupata vifaa vya kujifunzia ilikuwa kikwazo kikubwa kilichowafanya baadhi ya wanafunzi kushindwa kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya teknolojia duniani.
Wanafunzi wasioona, wenye uoni hafifu au wenye changamoto za kusikia walilazimika kutumia mbinu za kawaida za kujifunzia huku dunia ikiendelea kuhamia katika matumizi ya TEHAMA na kuwaacha nyuma.
Hata hivyo, hali hiyo inaendelea kubadilika kufuatia uwekezaji unaofanywa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote
(UCSAF), ambao umeanza kufikisha vifaa maalumu vya TEHAMA katika shule za wanafunzi wenye mahitaji maalumu nchini.
Hayo yameelezwa Mei 15,2026 Jijini Dodoma na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote nchini (UCSAF), Albert Richard kwenye mkutano maalum na wahariri wa vyombo vya habari mkoa wa Dodoma Kwa lengo la kujenga na kuimarisha mahusiano kati Yao na kuwezesha ushirikiano wa karibu na wa kudumu katika utekelezaji wa majukumu ya uhabarishaji umma.
Akizungumza kwenye mkutano huo ,amesema kupitia mradi wa Tehama, shule 22 tayari zimefikiwa na vifaa vya kisasa vinavyowasaidia wanafunzi kujifunza kwa urahisi zaidi, huku Serikali ikiweka mkakati wa kufikisha huduma hiyo katika shule nyingine 10 ndani ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Ametaja Vifaa vinavyotolewa kupitia mradi huo kuwa ni pamoja na mashine za Braille (Nukta Nundu), Orbit Readers, kompyuta mpakato, Embosser zinazotumika kuchapisha maandishi ya nukta nundu, Digital Voice Recorders pamoja na Magnifiers kwa wanafunzi wenye uoni hafifu.
"Shule zilizopata vifaa hivyo zinapatikana katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Dodoma, Mwanza, Katavi, Morogoro, Shinyanga, Ruvuma, Tabora, Arusha, Kagera, Mbeya, Njombe, Manyara, Mtwara, Rukwa, Kilimanjaro pamoja na Zanzibar,"amesema.
Amefafanua kuwa kupitia uwekezaji huo wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 1.84 hadi kufikia Juni 2025, wanafunzi wengi wenye mahitaji maalumu wameanza kupata fursa sawa ya elimu ya kidigitali kama ilivyo kwa wanafunzi wengine.
Mbali na kuwasaidia wanafunzi kujifunza kwa urahisi,amesema vifaa hivyo vitaongeza ari ya kujifunza, kujiamini pamoja na kuwapa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika masomo yanayotumia teknolojia.
Katika hatua nyingine,amesema UCSAF imepanga kupeleka vifaa hivyo katika shule nyingine 10 zikiwemo Musoma Tech mkoani Mara, Mustafa Sabodo ya Mtwara, Malangali ya Iringa, Buhongwa ya Mwanza, Tanga Tech pamoja na Kigoma Girls.
Hatua hiyo inaonyesha dhamira ya Serikali kuhakikisha mapinduzi ya kidigitali hayamuachi nyuma mwanafunzi mwenye uhitaji maalumu.
Hatua hizo zote zinaonyesha namna Serikali kupitia UCSAF inavyoendelea kujenga Tanzania ya kidigitali inayolenga kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za mawasiliano bila kujali eneo analoishi au hali yake ya kiafya.
Kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, miradi hiyo siyo tu uwekezaji wa teknolojia, bali ni daraja jipya la matumaini, usawa wa elimu na fursa za maisha bora katika dunia ya kidigitali inayokua kwa kasi.
Sambamba na hilo, UCSAF imeendelea kuwekeza katika miradi mbalimbali ya mawasiliano nchini kwa lengo la kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wote hususan waliopo maeneo ya vijijini na yasiyo na mvuto wa kibiashara kwa kampuni binafsi.




Social Plugin