Na Dotto Kwilasa, Dodoma
KAIMU Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote nchini (UCSAF), Albert wa amesema mfuko huo umeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano, TEHAMA na redio jamii katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuhakikisha wananchi wote, hususan wa vijijini, wanapata huduma za kidigitali.
Hayo yameelezwa Jijini hapa Mei 15,2026 kwenye wa mkutano maalum wa UCSAF na wahariri wa vyombo vya habari mkoa wa Dodoma Kwa lengo la kujenga na kuimarisha mahusiano kati yao na kuwezesha ushirikiano wa karibu na wa kudumu katika utekelezaji wa majukumu ya uhabarishaji umma
Akizungumza kwenye mkutano huo amesema UCSAF imefanikiwa kutekeleza miradi ya minara ya mawasiliano katika wilaya mbalimbali nchini, ambapo maeneo yaliyokamilika ni pamoja na Ngara mkoani Kagera, Kyela (Mbeya), Kisaki (Morogoro), Ngorongoro (Arusha), Makete (Njombe), Mbinga (Ruvuma) pamoja na Uvinza mkoani Kigoma.
Aidha,ametaja miradi mingine inayoendelea kutekelezwa katika maeneo ya Chemba (Dodoma), Chunya (Mbeya), Kiteto (Manyara), Rombo na Usangi (Kilimanjaro), Kaliua (Tabora), Nachingwea (Lindi), Mafia (Pwani), Newala na Nanyumbu (Mtwara) pamoja na maeneo mengine nchini.
Katika kuimarisha upatikanaji wa habari kwa jamii, amesema UCSAF pia inaendelea kutekeleza mradi wa kuboresha na kuanzisha redio jamii kupitia ujenzi wa studio, minara ya kurushia matangazo pamoja na usambazaji wa vifaa vya kisasa vya utangazaji.
Kupitia mradi huo, ujenzi wa minara na studio umekamilika katika maeneo ya Mtama (Mtwara), Kondoa (Dodoma), Kasulu (Kigoma), Same (Kilimanjaro), Rufiji (Pwani) na Kilindi (Tanga), huku baadhi ya miradi ikiendelea katika Bariadi, Kilosa, Mafia na Jiji la Dodoma.
Albert amesema UCSAF pia imeendelea kusaidia sekta ya elimu kwa kupeleka vifaa vya TEHAMA katika shule za umma, ambapo shule 1,121 zimenufaika na mradi huo unaojumuisha vifaa vya TEHAMA pamoja na ujenzi wa maabara.
Amesema hadi kufikia Juni 2025, Serikali kupitia UCSAF imewekeza zaidi ya Sh bilioni 5.94 katika utekelezaji wa mradi huo, huku shule nyingine 246 zikitarajiwa kunufaika kupitia bajeti ya mwaka 2024/25 na 2025/26.
Kwa upande wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, amesema UCSAF imepeleka vifaa maalumu vya kujifunzia katika shule 22 nchini, ikiwemo mashine za nukta nundu, Orbit Readers, kompyuta mpakato, vifaa vya kurekodi sauti pamoja na vifaa vya kukuza maandishi.
“Lengo letu ni kuhakikisha hakuna Mtanzania anayeachwa nyuma katika mapinduzi ya kidigitali. Tunaendelea kupeleka huduma za mawasiliano, intaneti na TEHAMA katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara,” amesema Albert.
Aidha, amesema UCSAF imeendelea kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu na wanafunzi wa kike kupitia mpango wa Girls in ICT Day, pamoja na kuanzisha huduma za bure za intaneti katika maeneo ya umma ikiwemo Sabasaba Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Tabora na Zanzibar.
Katika hatua nyingine, UCSAF inaendelea na mradi wa kuongeza uwezo wa minara 62 kutoka teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G ili kuboresha huduma za intaneti vijijini. Amesema minara 37 inayotekelezwa na kampuni ya Vodacom Tanzania tayari imekamilika kutoa huduma huku mingine ikiendelea chini ya TTCL.
Amesema UCSAF itaendelea kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na wadau mbalimbali kuhakikisha Tanzania inaendelea kufikia malengo ya uchumi wa kidigitali na upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wote.
Kwa upande wake, Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa UCSAF, Celina Mwakabwale amesema uelewa mdogo wa masuala ya kitaalam pamoja na uchochezi na upotoshaji wa taarifa bado ni changamoto kubwa inayokwamisha utoaji sahihi wa habari kwa umma.
Amesema baadhi ya taarifa zinazorushwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii hukosa usahihi kutokana na baadhi ya waandishi au wachambuzi kutokuwa na uelewa wa kina wa masuala ya kitaalam wanayoyazungumzia.
“Ni muhimu kwa waandishi wa habari kujenga uwezo wa kuelewa masuala ya kitaalam ili kuepusha upotoshaji wa taarifa ambao unaweza kuleta taharuki au migogoro katika jamii,” amesema Celina.
Aidha, ameonya kuhusu ongezeko la taarifa za uchochezi zinazoweza kuathiri amani na mshikamano wa jamii, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya taaluma ya habari pamoja na kufanya uhakiki wa taarifa kabla ya kuzichapisha au kuzirusha.
Baadhi ya washiriki wa semina hiyo wameeleza kuwa kuna haja ya kuendelea kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo wa kuchakata na kuwasilisha taarifa kwa weledi zaidi.
Mmoja wa Washiriki hao Hamida Ramadhan amesema waandishi wa habari Wana wajibu wa kufikisha ujumbe sahihi Kwa jamii kuhusu masuala ya TEHAMA ili kuepusha upotoshaji ambao unaweza kuleta taharuki kwenye jamii .
Semina hiyo imewakutanisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali pamoja na wadau wa sekta ya mawasiliano kwa lengo la kujadili namna bora ya kukabiliana na changamoto za upotoshaji wa taarifa nchini.


Social Plugin