Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUENDELEA KUTEKELEZA MIRADI YA KILIMO NA UVUVI



Na Mwandishi wetu – Dar es Salaam

Serikali imeeleza hazma yake ya kuendelea kutekeleza miradi ya mashirikiano katika sekta za kilimo na Uvuvi kwa pande mbili za Muungano ili kuongeza Ajira, uzalishaji mali, kuboresha usalama wa chakula, kuongeza thamani ya mazao, na kukuza Uchumi wa Buluu.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na wenye Ulemavu mh.Prof. Paramagamba Kabudi katika kikao cha ngazi ya Mawaziri cha Mashirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu Mtaa wa Magogoni Jijini Dar es Saalaam leo Tarehe 17 Mei 2026.

Azingumzia Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) inayotekelezwa na pande zote Mbili za Muungano, Profesa Kabudi amesema Serikali itaimarisha ushiriki katika sekta ya uvuvi wa Bahari kuu kwa kuwezesha mashirika ya uvuvi (TAFICO) kwa Tanzania Bara na (ZAFICO) kwa upande wa Zanzibar kwa kuwezeshwa kujenga meli sita za uvuvi sambamba na ujenzi wa viwanda vya kuchakata Samaki ambapo kwa upande wa Tanzania Bara kiwanda hicho kitajengwa katika wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi na Zanzibar katika eneo la Fungurefu.

Aidha, kwa upande wa Utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi alisema kuwa, Serikali imejiandaa kutoa taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya chama hicho ya nusu mwaka kwa pande zote mbili za Muungano ifikapo mwezi Julai, 2026 na taarifa ya mwaka mzima ifikapo mwezi Novemba 2026.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi wa Makamu wa Pili wa Rais anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe. Hamza Hassan Juma alisema Watanzania wengi wanajishughulisha na masuala ya kilimo hivyo kikao hicho kimeweza kuzungumzia fursa zinazopatikana katika sekta hizo zinazoratibiwa na ofisi hizo na kuongeza kuwa mafanikio mengi yanategemewa kupatikana katika vikao hivi vya mashirikiano.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com