Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeendesha mafunzo maalum kuhusu mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa wanakituo wa Taarifa na Maarifa wa Kata ya Kalenga mkoani Iringa.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mwendelezo wa semina zinazolenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu ukatili wa kijinsia na kuwahamasisha wanawake kushiriki kikamilifu katika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mafunzo hayo, mwezeshaji wa mafunzo, Scholastica Makwaia, alisema kuwa lengo kuu la semina hiyo ni kuwawezesha wanakituo kupata uelewa mpana kuhusu ukatili wa kijinsia, aina zake, athari zake kwa jamii pamoja na mbinu mbalimbali za kuuzuia na kuupambana nao.
Makwaia alieleza kuwa tangu kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo katika Kata ya Kalenga, mafanikio makubwa yameanza kuonekana, hususan katika kuwainua wanawake kijamii na kisiasa. Alisema wanawake wengi sasa wameanza kujitokeza kwa ujasiri kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, jambo ambalo hapo awali halikuwa la kawaida katika eneo hilo.
“Tunashuhudia mabadiliko chanya katika jamii. Wanawake wameanza kutambua uwezo wao na kuthubutu kushiriki katika maamuzi na nafasi za uongozi, jambo linalochangia maendeleo ya jamii kwa ujumla,” alisema Makwaia.
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo waliishukuru TGNP kwa kuendelea kutoa elimu muhimu inayosaidia kupambana na ukatili wa kijinsia. Walisema mafunzo hayo yamewaongezea maarifa, kujiamini na kuwajengea uwezo wa kuwa mabalozi wazuri wa kuelimisha jamii kuhusu haki za wanawake na umuhimu wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Washiriki hao walieleza kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kuhamasisha jamii zao kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuchangia kujenga mazingira salama, yenye usawa na fursa sawa kwa wanawake na wanaume.





















Social Plugin